Bikizee wa miaka 103 apona corona nchini Iran
Ajuza na bikizee wa miaka 103 aliyekuwa ameambukizwa kirusi cha corona amepona nchini Iran na ameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitalini.
Daktari Navid Danaei, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Afya cha mkoa wa Semnan wa kaskazini mwa Iran amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mtu mwenye umri mkubwa zaidi aliyepata ugonjwa wa COVID-19 mkoani humo ni bikizee wa miaka 103 ambaye Alhamdulillah hivi sasa amepona na ameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitalini.
Kabla ya hapo pia, babu mmoja mzee wa miaka 91 aliyekuwa ameambukizwa kirusi cha corona na ambaye pia alikuwa na matatizo mengine mengi kama ya moyo, shinikizo la damu na pumu katika mji wa Bam wa kusini mashariki mwa Iran, naye alipowa ugonjwa wa COVID-19 na kuruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa ya leo Jumatano ya Wizara ya Afya ya Iran, hadi hivi sasa wagonjwa 5,710 wa kirusi cha corona au COVID-19 wameshapona humo nchini kati ya watu 17,361 walioambukizwa ugonjwa huo hadi hivi sasa nchini Iran. 135 kati ya hao wamefariki dunia.
Juzi kwa mara nyingine Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alipongeza juhudi zisizo na kifani za watumishi wa sekta ya afya humu nchini katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kusema kuwa, takwimu na kiwango mapambano dhidi ya kirusi vya corona nchini Iran kinatia matumaini sana.