Jan 28, 2023 11:49 UTC
  • WHO: Vifo vitokanavyo na COVID-19 vinaongezeka, China inaongoza

Shirika la Afya Duniani, (WHO) limesema idadi ya vifo vinavyotokana na COVID-19 imeanza kuongezeka duniani tangu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Desemba.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Kimataifa ya WHO, kuhusu dharura za magonjwa ambacho kimekutana Ijumaa kwa mara ya 14 kutathmini iwapo bado COVID-19 ni dharura ya afya ya umma au la, wakati huu ambapo wiki ijayo mlipuko na maambukizi ya ugonjwa huo utaingia mwaka wa nne.

Amesema kuondolewa kwa vizuizi nchini China kumesababisha ongezeko la vifo kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani.

Dkt. Tedros amesema, “Wiki iliyopita vifo takribani 40,000 vya COVID-19 viliripotiwa WHO na zaidi ya nusu ni kutoka China.

Kwa  ujumla amesema katika wiki nane zilizopita, zaidi ya watu 170,000 waliaga dunia kwa COVID-19 duniani kote na idadi halisi inaweza kuwa kubwa.

Mkuu huyo wa WHO amesema chanjo, tiba na hatua zingine za kiafya dhidi ya COVID-19 bado ni hatua muhimu katika kuzuia ugonjwa huo na kuokoa maisha ya watu.

Dkt. Tedros amesema hatua za kimataifa bado zinasuasua kwa sababu katika nchi nyingi, hatua hizo muhimu za kuokoa maisha bado hazijawafikia wale wanaohitaji zaidi, kama wazee na wahudumu wa afya.

Amefafanua kuwa mifumo mingi ya afya duniani kote bado haina uwezo kamili wa kukabiliana na COVID-19, kando ya kuhudumia wagonjwa wenye matatizo mengine kama vile homa ya mafua makali, wakati huu ambapo kuna uhaba wa watumishi na hata walioko wamechoka.

Dkt. Tedros ametaja changamoto nyingine kuwa ni ufuatiliaji ambao umezorota huku imáni ya wananchi kwa mbinu za kinga kama vile chanjo ikiendelea kutikiswa na msururu wa taarifa potofu na za uongo.

Jumatatu tarehe 30 mwezi Januari, itakuwa miaka mitatu tangu COVID-19 itangazwe kuwa dharura ya afya ya umma duniani na hivyo kikao cha Ijumaa kitamshauri Dkt. Tedros iwapo dharura hiyo iendelee au la.

Tags