Iran: Nguvu na ushawishi wa jeshi letu la SEPAH ndio unaoihamakisha Marekani
Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran ametoa ujumbe kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Husain AS ambayo hapa nchini Iran inajulikana pia kwa jina la "Siku ya Pasdar" yaani Siku ya Ulinzi na kusema kuwa, nguvu na ushawishi wa kiistratijia wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ndiyo sababu ya kuhamaki, kudhalilika na kutengwa Marekani na maadui wengine ulimwenguni.
Katika ujumbe wake huo alioutuma kwa Brigedia Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iran amesema, kizazi cha hivi sasa cha jeshi la SEPAH kimerithi uzoefu wa miaka 40 wa wanajeshi mashujaa, waliojitolea vilivyo katika njia ya haki, waasisi na waliokuwa mstari wa mbele kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu katika vizazi vya mwanzo vya jeshi hilo.
Ujumbe wa Meja Jenerali Baqeri umeongeza kuwa, katika kipindi cha migogoro mizito, kipindi cha kiza na kipindi kisichotabirika, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH, liliweza kufanikisha malengo ya taifa la Iran kwa mkakati na stratijia yake maalumu kiasi kwamba matunda ya stratijia hiyo yanaonekana hadi leo katika anga ya kimataifa yakiwa na ujumbe wa kupigania haki, muqawama na kupambana na uistikbari.
Kamanda Meja Jenerali Baqeri vile vile amesema, kila leo Mapinduzi ya Kiislamu yanashuhudia kuchanua mafanikio mapya ya muqawama na kuzidi kurindima moto wa hasira za walimwengu dhidi ya ubeberu na uzayuni kiasi kwamba sasa hivi bendera ya kupambana na Marekani inaonekana kupepea katika kona zote za jiografia ya ubinadamu.
Mwezi 3 Shaaban ni siku ya kukumbuka kuzaliwa Imam Husain AS, Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia. Siku hii inajulikana kwa jina la "Siku ya Pasdar" hapa nchini Iran.