Maambukizi ya corona yapungua katika mikoa 16 nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60371-maambukizi_ya_corona_yapungua_katika_mikoa_16_nchini_iran
Naibu Waziri wa Afya nchini Iran amesema mkondo wa kupungua maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona unashuhudiwa katika mikoa 16 nchini Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 14, 2020 23:06 UTC
  • Maambukizi ya corona yapungua katika mikoa 16 nchini Iran

Naibu Waziri wa Afya nchini Iran amesema mkondo wa kupungua maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona unashuhudiwa katika mikoa 16 nchini Iran.

Iraj Harirchi, Naibu Waziri wa Afya wa Iran ameyasema hayo katika kikao alichokuwa nacho jana Jumanne na kuongeza kuwa: "Katika asilimia 25 ya mikoa ya Iran kiwango cha maambukizi mapya kila siku ni baina ya sifuri na 10 na katika asilimia 25 ya mikoa mingine kiwango hicho ni baina ya 10 na 20.

Harirchi aidha amesema kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, waliopoteza maisha kutokana na corona ni chini ya 100 kwa siku. Ameendelea kusema kuwa: "Kote nchini Iran kwa ujumla kunashuhudiwa kupungua kwa kiasi idadi ya maambukizi mapya ya corona."

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumanne ya Wizara ya Afya ya Iran, hadi sasa watu 74,877 wameambukizwa corona kote Iran na miongoni mwao 48,129 wamepata nafuu na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Aidha taarifa hiyo imesema katika kipindi cha masaa 24 hadi jana adhuhuri, watu 98 walikuwa wamepoteza maisha kutoka na corona nchini Iran na kwa msingi huo jumla ya waliopoteza maisha hadi sasa kote Iran kutokana na ugonjwa huo ni 4,683.