Abbas Mousavi: Vikosi vya kigeni visiilazimishe Iran kutoa onyo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60489-abbas_mousavi_vikosi_vya_kigeni_visiilazimishe_iran_kutoa_onyo
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa jibu kwa madai ya Marekani kuhusiana na doria ya vikosi vya ulinzi vya taifa hili katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kwamba, vikosi vya kigeni visiilazimishe Iran kutoa onyo na ukumbusho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2020 07:18 UTC
  • Abbas Mousavi: Vikosi vya kigeni visiilazimishe Iran kutoa onyo

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa jibu kwa madai ya Marekani kuhusiana na doria ya vikosi vya ulinzi vya taifa hili katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kwamba, vikosi vya kigeni visiilazimishe Iran kutoa onyo na ukumbusho.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari kwa njia ya video na kubainisha kwamba, uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo la Ghuba ya Uajemi ndio sababu ya kuvurugika amani na usalama wa eneo hili.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, kwa maelfu ya miaka sasa Iran imekuweko katika Ghuba ya Uajemi na kwamba, usalama wa eneo hili umekuwa ukidhaminiwa na kusimamiwa na taifa hili pamoja na nchi za eneo hili hususan Oman katika Lango Bahari la Hormoz.

Iran ikisimamia usalama katika Lango Bahari la Hormuz

Aidha Abbas Mousavi amesema kuhusiana na kufikia tamati vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA na juhudi za Marekani za kuongezwa muda wa vikwazo hivyo na kubainisha kwamba, serikali ya Washington inataka kuzipotosha fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusiana na ugaidi wa kiuchumi iliouanzisha.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hali ya mambo nchini Afghanistan na hatua zilizochukuliwa na Tehran kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi hiyo na kusema kuwa, Tehran inataka Afghanistan iliyo na amani na usalama na inataka kuundwe nchini humo serikali ya  jumuishi ambayo itasaidia kupatikana amani na uthabiti wa nchi hiyo.