Kamanda Hajizadeh: Leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola kubwa
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, leo hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dola kubwa na kwamba Marekani haiwezi kulifanyia upuuzi wowote taifa kubwa la Iran.
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mahojiano na Kanali ya Pili ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, teknolojia ya anga za mbali iliyo nayo Iran hivi sasa inazidi kupiga hatua siku baada ya siku na hakuna nchi yoyote yenye uthubutu wa kuichokoza Jamhuri ya Kiislamu.
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amezungumzia pia mashambulizi ya makombora ya Iran katika kambi ya wanajeshi magaidi wa Marekani ya Ain al Assad huko Iraq na kusema kuwa, siku ambayo Iran iliishambulia kwa makombora kambi hiyo, ilitarajia kuwa Marekani itajibu, lakini haikuthubutu kufanya hivyo.
Amezungumzia pia kurushwa katika anga za mbali satalaiti ya kwanza kabisa ya kijeshi ya Iran na kusema kuwa, kama Iran haitokuweko kwenye anga za mbali, itakuwa inakosa mambo mengi yanayohusiana na masuala ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi. Lakini hivi sasa na baada ya kufanikiwa kurusha satalaiti yake ya kwanza iliyopewa jina la "Nuru" ambayo inafanya kazi kwa ustadi mkubwa na inaizunguka dunia mara moja kila baada ya dakika 90, mafanikio hayo yataidhaminia Iran mahitaji yake mengi ya kiulinzi.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, juzi Jumatano lilirusha kwa mafanikio satalaiti yake iliyopewa jina la "Nuru" ikiwa ni mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutuma satalaiti ya kijeshi katika umbali wa kilomita 425 kutoka anga ya ardhi.