Kuheshimiwa dini za waliowachache nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60713-kuheshimiwa_dini_za_waliowachache_nchini_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ripoti ambayo hutolewa kila mwaka na Marekani kwa kisingizo cha uhuru wa kuabudu ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa msingi wa habari potofu, hivyo ameilaani ripoti hiyo na kusema haikubaliki kabisa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2020 03:49 UTC
  • Kuheshimiwa dini za waliowachache nchini Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ripoti ambayo hutolewa kila mwaka na Marekani kwa kisingizo cha uhuru wa kuabudu ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa msingi wa habari potofu, hivyo ameilaani ripoti hiyo na kusema haikubaliki kabisa.

Akiashiria ripoti hiyo ya kila mwaka ambayo hutolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusiana na hali ya uhuru wa kuabudu katika nchi tofauti za dunia, Abbas Musawi alisema jana Alkhamisi kwamba: Katika ripoti iliyotolewa hivi karibuni, kuna madai yasiyo na ukweli wala msingi kuhusu Iran. Madai hayo hayana ukweli wowote kuhusu dini yoyote ya kisheria na rasmi ya jamii za waliowachache katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivyo haikubaliki kabisa.

Kila mwaka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hutoa ripoti tofauti ambapo huzituhumu nchi tofauti za dunia, ikiwemo Iran, kuhusu mambo mbalimbali. Ripoti hiyo ya upande mmoja kuhusu uhuru wa kuabudu duniani ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imetajwa, inaonyesha wazi kuwa waliyoitayarisha hawatambui wala kudiriki vyema hali halisi ya mambo nchini Iran na kwamba wametetegemea maelezo na vyanzo visivyo na itibari na vilivyo dhidi ya Iran katika kuiandaa.

Ripoti hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu hali ya dini na madhehebu tofauti nchini  Iran iko mbali na ukweli wa mambo na vyanzo vilivyotegemewa katika kuitayarisha si vya kutegemewa wala kuaminika hata kidogo. Upitiaji wa haraka haraka tu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaonyesha wazi kwamba kuheshimiwa haki za binadamu na dini tofauti za mbinguni ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa nchini hapa.

Moja ya makanisa ya waliowachache nchini Iran

Kwa msingi wa katiba hiyo, jamii za wachache kidini zinatambuliwa rasmi kote nchini. Kwa ibara nyingine ni kuwa Wakristo, Wazartoshi na Mayahudi nchini Iran wana haki sawa na raia wengine wa nchi hii. Katiba ya Jamhuri y a Kiislamu ya Iran inasisitiza sana juu ya kuheshimiwa haki za binadamu za raia wa dini za waliowachache na jamii hizo za waliowachache pia zinawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamuri ya Kiislamu ya Iran.

Ili kujua zaidi uhuru wa shughuli za dini za waliowachache nchini, tunapasa kuzingatia kifungu cha 13 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kifungu hicho kinasema: Haki za raia wa dini za waliowachache wa Kizartoshi, Wakristo na Mayahudi nchini Iran zimebainishwa wazi na mbali na shughuli za kiuchumi, kidini na kiutamaduni pia wana nafasi katika chaguzi na utungaji wa sheria za nchi.

Katika uwanja huo Jonathan Bet Klia, mjumbe wa dini ya Waashuri (Waasyria) katika Bunge la Iran anasema: Hakuna haja ya wanaodai kutetea haki za binadamu kuwahurumia wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran. Watu hao hutoa madai matupu ya kutetea demokrasia. Bila shaka, wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran wanaishi katika nchi ambayo katiba yake haibagui kati ya Wakristo na Waislamu.

Imam Khomeini (MA) daima alikuwa akisisitiza umuhimu wa kuheshimiwa haki za wafuasi wa dini za waliowachache nchini

Kwa mujibu wa Jonathan Bet Klia, Waashuri (Waasyria) wakiwa ni Wakristo, wameishi nchini Iran kwa zaidi ya miaka 200 sasa, na wameishi kwa amani na utulivu na wenzao wa Kiislamu chini kwa miaka 1400. Kukiri huko kunathibitisha wazi kwamba katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazingatia kwa njia maalumu haki za wafuasi wa dini tofauti za mbinguni na hivyo ripoti za upande mmoja na za kisiasa haziwezi kufunika ukweli wa mambo kuhusu maisha mazuri na ya amani pamoja na uhuru wa kufanya shughuli tofauti za kisiasa, kiuchumi na kidini za wafuasi wa dini za waliowachache nchini hapa.

Historia inaonyesha wazi kwamba tokea zama za kale, Iran imekuwa mwenyeji wa dini, kaumu, makabila na tamaduni tofauti. Maisha ya amani, utulivu na urafiki baina ya makabila, makundi na wafuasi wa dini tofauti nchini Iran yana mizizi katika historia yake tajiri, jambo ambalo halionekani sehemu yoyote ile duniani, hata Marekani kwenyewe, ambayo inatoa matamshi na madai ya uongo kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kuabudu.