Upinzani DRC wamtaka Tshisekedi kuachana na mpango wa kubadili katiba
-
Rais Felix Tshisekedi
Kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amemtaka Rais Felix Tshisekedi kuachana na mapendekezo ya kufanyia marekebisho katiba ambayo wapinzani wanahofia yanaweza kutoa mwanya kwa rais huyo kugombea muhula wa tatu wa urais.
Delly Sesanga, rais wa chama cha ENVOL na mwanachama wa muungano wa upinzani wa C64, amesema kipaumbele cha upinzani ni kuhakikisha Tshisekedi anaondoka madarakani wakati muhula wake wa pili na wa mwisho utakapokamilika mwaka wa 2028.
"Mapambano tuliyonayo leo ni kuzuia mabadiliko yoyote ya katiba, kusimamisha muhula wa tatu kwa Bw. Tshisekedi, kusema apende asipende, mwaka wa 2028 hatakuwa na mamlaka tena ya kuongoza nchi yetu na lazima ang'atuke; lazima tuandae uchaguzi ili kuchagua viongozi wapya kwa ajili ya nchi," amesema Delly Sesanga.
Tshisekedi, ambaye amekuwa madarakani tangu 2019, alishinda muhula wa pili wa miaka mitano katika uchaguzi wa 2023. Kwa mujibu wa katiba ya sasaya Congo DR, Felix Tshisekedi hawezi kugombea muhula mwingine.
Mjadala kuhusu marekebisho ya katiba unakuja huku nchi hiyo ikiendelea kukumbwa na migogoro, hasa katika maeneo ya mashariki, ambapo kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda linadhibiti maeneo makubwa ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu.
Akizungumzia suala hilo, kinara wa upinzani, Delly Sesanga anasema juhudi zozote za kufikia amani ya kudumu lazima zijumuishe pande zote za mzozo, ikiwa ni pamoja na M23 na wanasiasa wa upinzani wanaoishi nje ya nchi.
Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika mwaka wa 2028 huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, upinzani unataka kuzidisha mashinikizo dhidi ya hatua yoyote ya kubadili katiba na kutaka mchakato jumuishi wa kisiasa ili kushughulikia migogoro ya usalama na kiuchumi nchini humo.