Zarif: Muibuaji mkubwa zaidi wa vita duniani anaiogopa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Marekani ni muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani na pia ina bajeti ya juu zaidi ya kijeshi kati ya mataifa yote ya dunia lakini pamoja na hayo ina wasi wasi kuhusu Iran kuondolewa vikwazo vya silaha."
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumamosi ambao ameuambatanisha na vidio inayoonyesha kiwango cha silaha ambazo Mareani inaziuza katika nchi zingine duniani. Katika ujumbe wake, Zarif amesema kuwa: "Kwa muda mrefu sasa Marekani imekuwa ikiongoza duniani katika bajeti ya kijeshi, uuzaji silaha, uibuaji vita na chokochoko na pia imekuwa ikifaidika sana na mapigano."
Zarif ameendelea kukumbuhsa kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ana wasi wasi mkubwa sana kuhusu Iran, nchi ambayo hadi kufikia mwaka 1979, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ilikuwa mnunuzi mkubwa wa silaha za Marekani. Ameongeza kuwa Pompeo ana wasi wasi mkubwa kuhusu Iran kiasi kwamba hivi sasa anamimina silaha kote duniani.

Siku ya Ijumaa, Pompeo alidai kuwa mapatano ya nyukla ya Iran maarufu kama JCPOA, ni mabovu na kuongeza kuwa, Marekani itatumia uwezo wake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa azimio la kuizia Iran kununua na kuuza silaha linaendelea kutetelezwa baada ya muda wake kumalizka.
Katika miaka ya 2006 na 2007 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea Iran marufuku ya kuuza na kununua silaha.
Kufuatia hatua ya Baraza la Usalama kupitisha mapatano ya JCPOA, iliafikiwa kuwa Okotaba 18 2020 Iran itaondolewa vikwazo vya silaha baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuidhinisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani.
Hivi sasa Marekani inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa marufuku hiyo haiondolewi. Marekani inadai kuwa ina wasi wasi kuhusu kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran katika hali ambayo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm imebaini kuwa Marekani ni muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani.