Shamkhani: JCPOA itakufa kikamilifu iwapo vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vitarefushwa
(last modified Sun, 03 May 2020 08:16:10 GMT )
May 03, 2020 08:16 UTC
  • Shamkhani: JCPOA itakufa kikamilifu iwapo vikwazo vya silaha dhidi ya Iran vitarefushwa

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameonya kuwa, iwapo azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakiukwa kwa kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran, basi makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatakufa daima.

Ali Shamkhani amesema hayo katika ujumbe alioutuma mapema leo kwenye ukurasa wa Twitter na kubainisha kuwa, "kuendeleza marufuku ya silaha dhidi ya Iran muda wake ukitamatika kutakuwa ni ukiukaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN."

Amezihutubu nchi za Ulaya kwa kusema, "Ulaya inasimama upande gani? Je itadumisha hadhi na heshima na kuimarisha maamuzi ya pande kadhaa, au itakubali kudhalilishwa na kuunga mkono uamuzi wa upande mmoja?"

Ali Shamkhani amesisitiza kuwa, lengo la Marekani la kushupalia mkakati wake wa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran ni  kuyumbisha irada na imani ya mrengo imara na unaopambana na uistikbari wa dunia. 

Baraza la Usalama la UN

Amesema 'virusi vya vikwazo' ni chombo kinachotumiwa na Ikulu ya White House ya Marekani kujaribu kuubakisha hai utawala wa kiistikbari wa Marekani unaoporomoka.

Baada ya Baraza la Usalama la UN kupitisha mapatano ya JCPOA, iliafikiwa kuwa Oktoba 18 mwaka 2020 Iran itaondolewa vikwazo vya silaha kwa ridhaa ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, jambo ambalo linaikera Washington.

Tags