Mousavi: Iran itatoa jibu kali endapo vikwazo vya silaha dhidi yake vitarefushwa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali endapo vikwazo vya silaha dhidi yake vitarefushwa.
Sayyid Abbas Mousavi ametoa kauli hiyo leo katika mkutano na waandishi wa habari alipoashiria hatua inazochukua Marekani kutaka vikwazo vya silaha ilivyowekewa Iran virefushwe; na akasisitiza kwamba, ikiwa vikwazo vya silaha vitarefushwa, Iran itachukua hatua kulingana na mazingira na kutoa jibu kwa hatua hiyo.
Msemaji wa chombo kikuu cha diplomasia cha Iran amebainisha kuwa, Marekani haiwezi kufikia lengo lake inalofuatilia hivi sasa, kwa sababu matakwa yake hayana msingi wa kisheria na nchi hiyo si mwanachama tena wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Mousavi amezungumzia pia mashtaka iliyofungua Iran kwa sababu ya hatua ya Ujerumani wakati wa Vita vya Kualazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran katika miaka ya 1980, ya kuuzia silaha za kemikali utawala wa Kibaathi wa dikteta wa Iraq Saddam; na akaeleza kwamba, Ujerumani imechangia sehemu kubwa ya jinai alizofanya Saddam dhidi ya wananchi wa Iran na hata wananchi madhulumu wa Iraq.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria pia harakati mpya za magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) nchini Iraq na lengo la kushambuliwa vikosi vya Al-Hashdu-Sha'abi ya nchi hiyo na akaeleza kwamba, Iran inafuatilia kwa karibu matukio ya Iraq na ina wasiwasi wa kufufuliwa upya makundi ya kigaidi na ukufurishaji nchini humo na hasa DAESH.
Sayyid Abbas Mousavi amesisitiza kuwa, Marekani inaandamwa na mashinikizo ya wananchi wa Iraq, hivyo inataka kuliimarisha kundi la Daesh ili ikwamishe mchakato wa kuondolewa askari wake nchini Iraq au icheleweshe muda wa kuondoka askari hao nchini humo.
Kuhusiana na hatua ya Ujerumani ya kuiweka Hizbullah ya Lebanon kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Ujerumani ina deni la kihistoria kwa Wazayuni, kwa hivyo inaendelea kufanya kazi ya kulipa deni hilo.../