Zarif: Pompeo alisome kwa makini azimio 2231 la Baraza la Usalama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif ametoa tamko kuhusu jitihada za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo za kutaka kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusema: "Azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijatengana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA; Pompeo asome kwa makini kuhusu azimio 2231."
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumanne, Zarif amekosoa jitihada za Pompeo za kutaka kurefushwa zaidi muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kupitia azimio 2231 na kusema: "Marekani haina nafasi tena katika azimio hilo."
Zarif ameendelea kusema kuwa: "Pompeo anadhani kuwa azimio 2231 la Baraza la Usalama linajitegemea na halihusiani na mapatano ya JCPOA. Anapaswa kulisoma kwa makini azimio 2231"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kusema kuwa, Pompeo hajalisoma azimio hilo na kuongeza kuwa: "JCPOA ni sehemu ya azimio 2231. Ni kwa sababu hii ndio azimio hilo lina kurasa 104 na hiyo ndiyo sababu ambayo imempelekea Pompeo asilisome."
Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hivi karibuni alidai kuwa, Marekani ni mshirika katika azimio 2231 na inaweza kuomba kurefushwa muda wa vikwazo dhidi ya Iran.

Vikwazo vya silaha vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa viliwekwa katika miaka ya 2006 na 2007 ambapo linaizuia Iran kununua au kuuza silaha.
Kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa Oktoba 18 2020 baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuthibitisha kuwa shughuli za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani.