Karibu watu 83 elfu wapona corona nchini Iran
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa 82 elfu na 744 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran ametangaza hayo leo Alkhamisi katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa wagonjwa wapya 1,485 wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia leo mchana watu laki moja na 3,135 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.
Daktari Jahanpur halikadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 68 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo mchana na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,486 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran aidha amesema, kufikia sasa karibu vipimo laki tano na 45,000 vya corona vimeshafanyiwa uchunguzi nchini Iran na kuongeza kuwa, thuluthi mbili ya wagonjwa wapya ni katika watu waliokaa karibu na wagonjwa au familia za wagonjwa hao.
Idadi ya walioambukizwa corona duniani kote hadi leo mchana ilikuwa ni zaidi ya milioni 3 na laki nane na 43,187. Watu wasiopungua 265,657 wameshaaga dunia na wengine zaidi ya milioni moja na laki tatu na 14,421 wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.