Umuhimu wa utulivu wa kisiasa na usalama wa Iraq kwa Iran
Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuelezea kufurahishwa kwake na kuundwa serikali mpya nchini Iraq inaonesha kuwa utulivu wa kisiasa na usalama wa nchi hiyo kwa nchi jirani ya Iran ni muhimu sana.
Serikali mpya ya Iraq inayoongozwa na Mustafa al Kadhimi, Jumatano usiku ilipigiwa kura na kupasishwa na Bunge la nchi hiyo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa nchi ya kwanza kabisa jirani wa mashariki mwa Iraq kuelezea kufurahishwa kwake na hatua hiyo.
Iran ambayo daima ni jirani muhimu kwa Iraq inaunga mkono hatua za ndani ya nchi hiyo za kuimarisha utulivu na mshikamano, na muda wote imekuwa ikiheshimu maamuzi ya wananchi wa nchi hiyo. Msimamo huo wa Iran unaonesha ni kiasi gani Jamhuri ya Kiislamu inaheshimu msingi wa kuishi salama na majirani zake na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwani inatambua kuwa huo ndio msingi wa kuwa na uhusiao mzuri na wa kibunifu baina ya nchi jirani.
Mataifa mawili ya Iran na Iraq yana hali moja za kiutamaduni, lugha, dini na mpaka mrefu wa pamoja hivyo zinaathiriana sana na kwamba uhusiano wa nchi hizi mbili, msingi wake mkuu ni wananchi wenyewe wa nchi hizo. Kila mwaka mamilioni ya wafanyaziara kutoka Iran na Iraq wanaingia katika nchi hizo mbili na hili linazidi kuonesha uhusiano wa damu na madhubuti wa kiutamaduni na kidini wa nchi hizi mbili, hivyo utulivu na usalama wa Iraq, bila ya shaka yoyote una umuhimu mkubwa kwa Iran.
Msimamo huo mkuu na muhimu katika siasa za mambo ya nje za Iran hasa msimamo wake mzuri kuhusu majirani zake ndio ulioifanya Tehran kuwa ya kwanza kulipongeza taifa la Iran kwa kufanikiwa kuunda serikali na kuimarishwa utulivu wa kisiasa nchini humo. Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Alkhamisi aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima iko pamoja na wananchi wa Iraq na serikali yao waliyoichagua kidemokrasia.
Iran inauhesabu usalama na utulivu wa Iraq kuwa ni sawa kabisa na usalama na utulivu wake bali pia ni usalama na utulivu wa eneo zima la Asia Magharibi hasa kwa kuzingatia hali ilivyo ya kijiografia na masuala mengi yanayoyaunganisha mataifa haya mawili. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana mara baada ya genge la kigaidi la Daesh (ISIS) kuivamia Iraq na kuteka maeneo yake kadhaa, Iran ilisimama imara kuwaunga mkono wananchi, serikali na jeshi la Iraq kupambana na genge hilo la ukufurishaji.
Hatua hiyo ya kiudugu na kiurafiki imeimarisha mno ushirikiano wa nchi hizi mbili na hivi sasa Iran na Iraq zina uhusiano imara kabisa katika nyuga zote ukiwemo uchumi.
Iran ina uwezo mkubwa wa kiuchumi katika sekta mbalimbali na kutokana na masafa madogo yaliyopo baina yake na Iran, serikali ya Baghdad inaweza kutumia vizuri sana fursa hiyo kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Rais Barham Saleh wa Iraq akasisitiza kwa kusema: Iran ni jirani muhimu kwa Iraq na kwamba nchi mbili hizi zina mpaka wa pamoja hivyo kulindwa uhusiano na Iran ni jambo muhimu sana kwa Iraq.
Msingi wa kuweko uhusiano mzuri na imara ni kuweko serikali madhubuti na imara na kwa vile jambo hilo ni kitu cha dharura, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono kuundwa serikali mpya ya Iraq sambamba na kuheshimiwa kura na maamuzi ya wananchi wa nchi hiyo.