Iran yautaka utawala wa Marekani ukomeshe ugaidi wake wa kiserikali
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu madai ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kwamba, eti Iran haijatoa ushirikiano katika kupambana na ugaidi na kusema kuwa, serikali ya Washington inapaswa kukomesha ugaidi wake wa kiserikali.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akijibu madai hayo ya kuchekesha ya Marekani na kusema wazi kwamba, kutokana na Washington kuwa na historia kongwe ya kuyadhamini na kuyapatia fedha na silaha makundi mbalimbali ya kigaidi, kutekeleza kwake ugaidi wa kiserikali na kuuunga mkono waziwazi utawala wa Israel unaofanya mauaji kila leo dhidi ya Wapalestina, nchi hiyo haiwezi kuwa kipimo kizuri cha kutathmini juhudi zilizofanyika kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, utawala wa Marekani daima na hususan katika miaka ya hivi karibuni umeyaunga mkono makundi ya kigaidi katika eneo hili la Asia Magharibi kama Daesh, mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na utawala bandia wa Israel.
Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imetoa tamko kuhusu siku ya "Nakba" yaani siku ya nakama ya kuasisiwa utawala pandikizi wa Kizayuni katika ardhi walizoporwa Wapalestina na kusisitiza kuwa, kadhia ya Palestina itaendelea kuwa suala kuu na nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu licha ya kufanyika njama nyingi za kulisahaulisha hilo.
Leo tarehe 14 Mei inasadifiana na mwaka wa 71 wa kufukuzwa mamia ya maelfu ya Wapalestina kwenye ardhi zao na kesho yaani tarehe 15 Mei, utawala pandikizi wa Kizayuni uliopachikwa jina bandia la Israel, utatimiza miaka 71 tangu kupandikizwa kwake kwenye ardhi hizo za Wapalestina.