Rais Rouhani: Nchi za Ulaya zisiishie kulaani tu, zichukue hatua za kivitendo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi za Ulaya zisiishie kulaani tu hatua zilizo kinyume cha sheria za Marekani, bali zitekeleze kivitendo majukumu yao.
Rais Rouhani amesema hayo leo Jumanne katika mazungumzo ya simu na Rais Sauli Niinistö wa Finland na kusisitiza kuwa, utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni sehemu ya kuimarisha kivitendo fikra ya ushirikiano wa pande kadhaa na kuongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kujitoa katika mapatano hayo kinapingana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama ambavyo ni kinyume na sheria za kimataifa, si uwajibikaji wa kisiasa na ni kudharau wajibu wa kimaadili wa watu wote wa kuheshimu ahadi wanazotoa.
Vile vile amesema, ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA unaendelea vizuri, hata hivyo amesema, inasikitisha kuona kuwa, Wamarekani wameshindwa kuonesha nia njema hata mara moja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, hata wakati wa kuenea kirusi cha corona, Wamarekani wameendelea kuliwekea vikwazo taifa la Iran na wamezuia kufika humu nchini dawa za dharura na hawakujali usalama wa Wairan milioni 83.
Amegusia pia kuanzisha mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kwa kifupi INSTEX na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba kanali za mabadilishano ya fedha za nchi za Ulaya zimeshindwa kuzaa matunda yaliyotakiwa hivyo Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua za kivitendo za kuzifanya kanali hizo kuwa amilifu zaidi.
Kwa upande wake, Rais Sauli Niinistö wa Finland amepokea vizuri kuanzishwa kanali ya mabadilishano ya fedha baina ya Ulaya na Iran maarufu kwa jina la INSTEX na kusema kuwa, mapatano ya JCPOA ni makubaliano ya kimataifa ambayo inabidi yalindwe na pande zote.