Jasusi wa CIA na Mossad ahukumiwa kifo nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61502-jasusi_wa_cia_na_mossad_ahukumiwa_kifo_nchini_iran
Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema kuwa, jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na shirika la ujasusi la Israel, Mossad hapa nchini, amehukumiwa kifo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2020 06:48 UTC
  • Gholamhossein Esmaili
    Gholamhossein Esmaili

Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema kuwa, jasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na shirika la ujasusi la Israel, Mossad hapa nchini, amehukumiwa kifo.

Gholamhossein Esmaili amewaambia waandishi habari mapema leo kwamba Mahmoud Mousavi-Majd ambaye ni miongoni mwa majasusi wa CIA na Mossad alikamatwa hapa nchini kutokana na hatua makini za askari usalama wa Iran.

Esmaeli ameongeza kuwa, jasusi huyo alikuwa akilipwa dola za kimarekani mkabala wa kutayarisha ripoti za kijasusi zinazohusiana na masuala ya usalama hususan vikosi vya jeshi la Iran, Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sehap) na mahala alipokuwa Meja Jenerali Qassem Soleimani na kuzikabidhi kwa mashirika ya ujasusi ya CIA na Mossad. Amesema jasusi Mahmoud Mousavi-Majd amehukumiwa kifo na Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kupatikana na hatia. 

Mahmoud Mousavi-Majd amehukumiwa kifo.

Msemaji wa Idara ya Mahakama za Iran amesema kuwa, hukumu hiyo imepasishwa na Mahakama Kuu ya Iran na itatekelezwa hivi karibuni. 

Kuhusiana na faili na ndege ya Ukraine iliyoanguka hapa nchini Ismaili amesema kuwa, hadi sasa wamekamatwa watu 6 kuhusiana na kadhia hii na mahakama ya Iran inafuatilia suala hili kwa nguuvu zote.