Iran: Bodi ya Magavana ya IAEA isithubutu kuchukua hatua isiyo na maana
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu mwafaka kwa hatua yoyote hasi na isiyo na maana itakayochukuliwa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya taifa hili, kwa kutegemea madai yasiyo na msingi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sayyid Abbas Mousavi ameyasema hayo leo Jumatatu katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari hapa jijini Tehran na kubainisha kuwa, "tunausa wakala huo (IAEA) uzingatie uhalisia wa mambo kwa kutegemea misingi ya sheria, na usijiingize katika masuala yasiyo na maana."
Amesema anatumai kuwa wakala huo hautaburuzwa kuchukua hatua isiyo na mantiki akisisitiza kwamba, IAEA inafamu vyema hatua ya kujibu mapigo itakayochukuliwa na Iran.
Mousavi amekumbusha kuwa, "Iran imeendelea kushirikiana na IAEA licha ya wakala huo kupunguza ushirikiano wake. Iwapo mwenendo huo utaendelea, itakuwa vigumu kuamiliana na shirika hilo (la nishati ya atomiki)."
Jana Jumapili pia, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikosoa kitendo cha Marekani cha kuzitishia Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki (IAEA) na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa maslahi ya Washington na kubainisha kuwa, Tehran itatoa jibu mwafaka iwapo kipengee muhimu cha kuondolewa Iran vikwazo vya silaha kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN kitakiukwa.
Baada ya kupitishwa azimio 2231 la Baraza la Usalama mwaka 2015, Iran ilipigwa marufuku kununua au kuuza zana aina saba za kivita ikiwa ni pamoja na vifaru, magari ya deraya, mizinga, ndege za kivita, helikopta, manoari na makombora. Vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Iran vinatazamiwa kuondolewa Oktoba 18 mwaka huu wa 2020, lakini Marekani inafanya juu chini kuhakikisha kuwa vinarefushwa.
Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki inatazamiwa kukutana leo Jumatatu kujadili ripoti zinazodai kuwa Iran imezuia kufanyika ukaguzi katika vituo vyake vya viwili ambako 'shughuli za nyuklia zimefanyika.'