Katika kuwakumbuka wahanga wote wa silaha za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i61896-katika_kuwakumbuka_wahanga_wote_wa_silaha_za_kemikali
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya wahanga wa silaha za kemikali hata hivyo haiko mbali siku moja serikali zile zilizouunga mkono utawala wa Saddam zikalazimika kuomba radhi mbele ya fikra za waliowengi kwa hatua zao za fedheha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 29, 2020 04:57 UTC
  • Katika kuwakumbuka wahanga wote wa silaha za kemikali

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya wahanga wa silaha za kemikali hata hivyo haiko mbali siku moja serikali zile zilizouunga mkono utawala wa Saddam zikalazimika kuomba radhi mbele ya fikra za waliowengi kwa hatua zao za fedheha.

Tarehe 28 Juni inasadifiana na kutimia mwaka wa 33 wa kukumbuka janga la kushambuliwa kwa silaha za kemikali mji wa Sardasht Iran. Utawala wa Baath wa Iraq tarehe 28 mwezi Juni mwaka 1987 uliushambulia kwa silaha za kemikali mji wa mpakani wa Sardasht nchini Iran.Watu 110 waliuliwa shahidi na wengine zaidi ya elfu nane walidhurika na silaha hizo za kemikali katika shambulio hilo. 

Wahanga wa silaha za kemikali za Saddam katika mji wa Sardasht, Iran 

Sambamba na siku hiyo chungu ambayo huadhimishwa katika kuwakumbuka wahanga wote wa silaha za kemikali; jana Jumapili kulifanyika mkutano hapa Tehran chini ya anuani " Ulinzi wa Kemikali." 

Serikali na mashirika mengi yalihusika kuupatia utawala wa Saddam silaha za kemikali katika kipindi cha mwaka 1980 hadi 1988, hata hivyo ni katika mwaka wa mwisho pekee wa vita na kulingana na kiasi cha silaha za kamikali zilizotumiwa na utawala vamizi wa Iraq ambapo Mwendesha Mashtaka wa Ujerumani aliwasilisha mashtaka dhidi ya mashirika kadhaa ya Kijerumani ambayo yalituhumiwa kutuma na kusambaza mada za kemikali kwa Iraq kwa ajili ya kuunda mabomu. Pamoja na hayo, faili la jinai hizo dhidi ya binadamu zilifuatiliwa na kushughulikiwa kwa msingi tu wa eti kukiukwa sheria za forodha; na wala hayakutajwa majina ya mashirika makuu ya Ujerumani yaliyohusika kuuandalia utawala wa Iraq mada, zana na teknolojia iliyokuwa ikihitajika. Saddam alitumia silaha za kemikali zaidi ya mara 250 katika vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran; vita ambavyo vilipelekea kuuliwa shahidi watu elfu nane na kujeruhi wengine 107,000.   

" Fernando Arias" Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Linalopiga Marufuku Silaha za Kemikali (OPCW) ametuma ujumbe kwa mnasaba wa kukumbuka shambulio la kemikali la utawala wa Saddam katika mji wa Sardasht na kubainisha masikitiko yake makubwa na kutoa pole kwa ndugu wa wahanga wa mashambulizi ya kemikali. Amesema katika kadhia hii raia wa Sardasht, wahanga wote na vizazi vijavyo wana haki kwetu. 

Fernando Arias, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la OPCW  

Mikataba ya kimataifa iliyopasishwa katika kalibu ya hati mbalimbali na kanuni na sheria za kimataifa imepiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali. Pamoja na hayo swali hili lingali linaulizwa kwamba je sheria za kimataifa pekee  zinaweza kujibu masuala haya?  

Protokali na maazimio mengi  ikiwemo Protokali ya mwaka 1925 ya Geneva yalisainiwa kwa lengo la kukabiliana na matumizi ya silaha za kemikali baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Katika kuendelezwa jitihada mbalimbali katika uwanja huo; azimio la kupiga marufuku matumizi ya silaha hizo (CWC) lilipasishwa tarehe Tatu Septemba 1992 baada ya miaka 20 ya mazungumzo na baada ya hapo  Shirika la Kupiga Marufuku Silaha za Kemikali (OPCW) mwaka 1997 huku likiwa na nchi wanachama 192 lilianza shughuli zake mwaka 1997 kwa nara  ya "Ushirikiano wa pamoja kwa ajili ya kuwa na dunia pasina na silaha za kemikali." 

 Licha ya kupasishwa mikataba hiyo lakini bado baadhi ya nchi ikiwemo Marekani haziheshimu wala kufungamana na ahadi na majukumu yake kwa mujibu wa maazimio hayo ya kimataifa. Taarifa ya mkutano wa jana wa Tehran ni dhahir shahir kwamba imeakisi sehemu ya ukweli huo mchungu wa mambo na wakati huo huo imesisitiza kufuatiliwa kisheria maslahi ya familia za mashahidi, wale wote waliopata ulemavu na wahanga wa silaha za kemikali na kuhukumiwa watenda jinai hizo. Taasisi za amani na wanaharakati dhidi ya silaha za maangamizi ya halaiki nchini Iran na ulimwenguni kwa ujumla wamefanya jitihada katika miaka yote hii kufikisha kwa walimwengu kwa njia mbalimbali ujumbe wa amani wa wahanga na majeruhi wa kemikali. Mkutano wa Taifa wa Tehran pia umefanyika kwa lengo hilo.  

Kama alivyoandika Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika ukurasa wake wa Twitter kwa mnasaba wa kumbukumbu ya maafa ya Sardasht kwamba: Kitendo cha utawala wa Saddam cha kutumia silaha za kemikali hakijaacha kitu kingine bali fakhari kwa wananchi wa Iran na fedheha,  aibu na  kulaaniwa daima wahusika wa jinai hizo.  

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambp ya Nje wa Iran