Mousavi: Viongozi wa Iran na China wameazimia kustawisha uhusiano wa kistratejia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa kwa mujibu wa mapatano ya mwaka 2016 kati ya Marais wa Iran na China, nchi mbili ziliweka wazi irada na azma yao ya kisiasa ya kustawisha na kupanua zaidi ushrikiano wa kistratejia na kuandaa ramani ya njia ya miaka 25 kati ya Tehran na Beijing ili kutayarisha uwanja mzuri wa ustawi wa pande zote katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi katika miaka ijayo.
Sayyid Abbas Mousavi aliyatamka haya jana Jumatano akijibu hujuma kubwa ya madai ya uwongo kuhusu ramani ya njia ya miaka 25 kati ya Iran na China.
Mousavi amesema kuwa rasimu ya mapatano ya awali ya ushirikiano wa Iran na China imeandaliwa kwa kuzishirikisha taasisi za kitaalamu za nchi mbili na hivi sasa rasimu hiyo inajadiliwa. Amesema, hati hiyo ya mapatano itawasilishwa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) baada ya kumalizika mazungumzo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria msimamo wa kihasama na ghadhabu ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mkabala wa makubaliano ya Iran na China na kueleza kuwa: Bila shaka uhusiano wa kistratejia wa Iran na China ambao una maslahi makubwa kwa ajili ya watu wa nchi mbili umewafanya maadui waanzishe njama za kufelisha mazungumzo hayo.
Mousavi ameyataja madai kama ya kukodishwa visiwa vya Iran katika Ghuba ya Uajemi kwa China, kuipatia Beijing haki ya kununua mafuta y Iran kwa bei ya chini na kutuma wanajeshi wa nchi hiyo katika ardhi ya Iran kuwa ni kichekesho na dhihaka ambayo haina thamani ya kukadhibishwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, anataraji mpango wa ushirikiano kati ya Tehran na Beijing utakamilika katika siku chache zijazo na amevitaka vyombo vya habari kujiepusha kuchapisha matini zinazoandaliwa kwa malengo mbalimbali ya kichochezi.