Iran na Syria zatiliana saini hati ya ushirikiano wa kijeshi na kiusalama
Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri wa Ulinzi wa Syria wametiliana saini mjini Damascus hati ya ushirikiano wa pande kadhaa katika nyanja za kijeshi, kiulinzi na kiusalama.
Meja Jenerali Muhammad Bagheri, Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ali Abdullah Ayyoub, Waziri wa Ulinzi wa Syria walitliana saini makubaliano hayo hapo jana na kusisitiza juu ya azma ya pande mbili ya kushirikiana kwa dhati katika nyuga hizo.
Maafisa hao wa ngazi za juu wa kijeshi na kiulinzi wa Iran na Syria wamesema kuwa, lengo la hati hiyo ya ushirikiano ni kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiufundi katika nyanja mbalimbali za shughuuli za kijeshi baina ya nchi mbili hizo.
Aidha pande hizo zimebainisha kuwa, hati hiyo inataka kuendelezwa uratibu baina ya pande mbili kwa ajili ya kukabiliana na changamoto na matishio mbalimbali yanayoongeza kila leo.
Meja Jenerali Muhammad Bagheri, Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ali Abdullah Ayyoub, Waziri wa Ulinzi wa Syria wametoa taarifa mwishoni mwa mazungumzo yao mjini Damascus wakisisitiza kuwa, kuendelezwa vita dhidi ya ugaidi wa kitakfiri unaoungwa mkono na baadhi ya madola ya eneo la Asia Magharibi na hata kimataifa ni miongoni mwa malengo ya hati hiyo ya ushirikiano.