Abdollahian: Utawala wa Aal-Khalifa uimarishe uhusiano wa Wabahrain, si Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62192-abdollahian_utawala_wa_aal_khalifa_uimarishe_uhusiano_wa_wabahrain_si_israel
Mshauri wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya kimataifa ameukosoa vikali utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain kwa kukanyaga haki za binadamu za raia wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2020 03:36 UTC
  • Abdollahian: Utawala wa Aal-Khalifa uimarishe uhusiano wa Wabahrain, si Israel

Mshauri wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya kimataifa ameukosoa vikali utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain kwa kukanyaga haki za binadamu za raia wa nchi hiyo.

Hossein Amir-Abdollahian, Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Iran amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, badala ya utawala wa Manama kuimarisha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel, unapaswa kurekebisha namna unavyoamiliana na wananchi wa Bahrain.

Amesema kitendo cha utawala wa Aal-Khalifa cha kuidhinisha hukumu ya kifo dhidi ya vijana wawili wa Kibahrain katika mazingira ya sasa ya janga la corona, kinaashiria wazi mpasuko mkubwa uliopo baina ya utawala huo na wananchi wa Bahrain.

Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali ukandamizaji, hukumu bandia za kifo na ukiukaji wa haki za binadamu wa kimfumo unaoshuhudiwa nchini Bahrain.

Ukandamizaji wa polisi ya Bahrain dhidi ya raia

Mshauri wa Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, utawala wa Aal-Khalifa unapaswa kuangalia upya namna unavyoamiliana na raia wa nchi hiyo, badala ya kufanya jitihada za kuboresha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Jana Jumatatu, vijana wawili wa Kibahrain ambao walikiri mashitaka dhidi yao baada ya kufanyiwa ukandamizaji wa kila namna, kwa mara ya tano walihukumiwa kifo, hatua ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yameitaja kama doa jingine kwenye rekodi ya dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Manama, dhidi ya wakosoaji wake.