Zarif: Serikali ya Trump imetengwa na kufedheheka tena katika medani ya kimataifa
-
Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia upinzani wa jamii ya kimataifa dhidi ya hatua ya Marekani ya kutaka kutumia vibaya taratibu zilizowekwa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA za kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran na kusema, kwa mara nyingine tena serikali ya Trump imetengwa na kufedheheka katika medani ya kimataifa.
Baada ya Marekani kuliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikitaka kutekelezwa taratibu zilizoainishwa kwenye makubaliano hayo ukiwemo ule unaojulikana kama "Utaratibu wa Kurejesha Papo kwa Papo" yaani "Snapback Mechanism", Muhammad Javad Zarif leo Ijumaa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Mike Pompeo anaona njozi kwamba amehuisha utaratibu wa "Snapback Mechanism", wa kurejesha vikwazo vilivyofutwa vya Baraza la Usalama la UN. Ameandika kuwa: Wakati huo huo Iran, Russia, China, Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimeliandikia barua tofauti Baraza la Usalama zikisema hatua ya serikali ya Trump inakiuka sheria na ni bure bilashi.
Zarif amesema kuwa, kuna uwezekano kwamba hii leo wanachama wengine wa Baraza la Usalama la UN pia watachukua msimamo kama huo, na serikali ya Donald Trump itatengwa na kufedheheka tena katika medani ya kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje Nchi za Nje wa Iran amesema: Historia ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haijawahi kushuhudia tukio kama hili.
Ijapokuwa miaka miwili nyuma Marekani ilitangaza rasmi kinyume cha sheria na bila kujali azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama uamuzi wa kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hivi sasa imeibuka na tafsiri nyingine mpya ya kisheria na kudai kwamba kwa mujibu wa vipengele vya azimio hilo ingali ni mdau katika JCPOA na kwa muktadha huo ina haki ya kutumia taratibu zilizoainishwa kwenye makubaliano hayo ukiwemo ule unaojulikana kama "Utaratibu wa Kurejesha Papo kwa Papo" yaani "Snapback Mechanism", ambao ni wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na Baraza la uisalama la Umoja wa Mataifa.
Russia, China Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zimepinga takwa hilo l Marekani