Araqchi: Wanachama wa JCPOA hawaitambui Marekani kama mshirika wao
(last modified Wed, 02 Sep 2020 03:31:22 GMT )
Sep 02, 2020 03:31 UTC
  • Araqchi: Wanachama wa JCPOA hawaitambui Marekani kama mshirika wao

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema nchi zilizosalia katika makubaliano ya nyuklia ya Iran haziitambui Marekani kuwa mwanachama au mshirika wa mapatano hayo ya kimataifa.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo akiwa Vienna, mji mkuu wa Austria alikoenda kushiriki kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA kilichofanyika jana Jumanne.

Ameeleza bayana kuwa: "Washirika wa Iran katika JCPOA hawaitambua tena Marekani kama mshirika wa makubaliano hayo na kwa msingi huo, (Washington) haina haki ya kutumia utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN unaofahamika kama 'Snapback Mechanism."

Sayyid Araqchi ameongeza kuwa, mjumuiko wa washirika wa makubaliano hayo ya kimataifa umetuma ujumbe ulio wazi kwa dunia juu ya msimamo wao.

Araqchi na Grossi walipokutana na kufanya mazungumzo jana mjini Vienna

Kadhalika hapo jana, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran alikutana pambizoni mwa kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi. Baada ya kikao cha wawili hao, Grossi aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, "(imekuwa) vyema kukutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran @Araqchi baada ya safari yangu ya Tehran. Kazi yetu lazima iendelee."

Iran na IAEA wiki iliyopita zilifanya mazungumzo yaliyokuwa na natija nzuri hapa mjini Tehran ambapo Iran ilifikia makubaliano mapya na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuhusiana na suala zima la kupanua ushirikiano.

Tags