Rais Rouhani: Marekani kamwe haitofikia malengo yake dhidi ya Iran
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia hatua za kiuadui zinazochukuliwa na Marekani kama vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran na kusema kuwa, viongozi wa Washington kamwe hawatofikia malengo yao haramu.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumatano kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri la serikali yake na kuongeza kwamba, Marekani ilikuwa inadhani kuwa kwa kuibebesha Iran mashinikizo ya kiuchumi italifanya taifa hili la Kiislamu lisalimu amri na kuipiga magoti White House, lakini si tu Washington imeshindwa kufikia lengo lake hilo bali pia imeaibika na kupoteza heshima mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mbele ya walimwengu na hata mbele ya wananchi wenyewe wa Marekani.
Vile vile amesema, maadui wa taifa la Iran wameanzisha kanali za uongo za habari ili kuendesha propaganda, kueneza uongo na kupiga vita kila jambo zuri la taifa la Iran. Si hayo tu, lakini pia kila siku kanali na mabanda hayo ya propaganda ya maadui yanatumia kila kisingizio kueneza hofu na ukatishaji tamaa katika nyoyo za Wairan lakini mara zote wananchi wa Iran wamekuwa macho na kufedhehesha njama hizo za maadui.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amewashukuru wananchi kwa kusimama imara mbele ya mashinikizo ya kiuchumi na vikwazo vya kidhalimu vya adui na amesema, wananchi, mihimili mikuu ya dola na viongozi wa taasisi zote za Iran wanatumia uwezo wao wote katika kipindi hiki kizito na licha ya kuweko matatizo mengi yaliyosababishwa na vikwazo na janga la corona, lakini Alhamdulillah, Iran imebakia salama na inaendelea mbele na ustawi wake wa kila namna ukiwemo wa kiuchumi.