Propaganda za kihabari na kisiasa za nyuma ya pazia dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63456-propaganda_za_kihabari_na_kisiasa_za_nyuma_ya_pazia_dhidi_ya_iran
Senario ya kuenea chuki dhidi ya Iran “Iranophobia” hadi sasa zimeendeshwa kwa kutumia maudhui mbalimbali kama uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya nchi nyingine katika eneo la Asia Magharibi, tishio la Tehran la nguvu za kijeshi, makombora na kuunga mkono ugaidi, ukiukaji wa haki za binadamu na kuzusha wasiwasi katika uga wa miradi ya nyuklia ya Iran inayofanyika kwa malengo ya amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 16, 2020 03:31 UTC
  • Propaganda za kihabari na kisiasa za nyuma ya pazia dhidi ya Iran

Senario ya kuenea chuki dhidi ya Iran “Iranophobia” hadi sasa zimeendeshwa kwa kutumia maudhui mbalimbali kama uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya nchi nyingine katika eneo la Asia Magharibi, tishio la Tehran la nguvu za kijeshi, makombora na kuunga mkono ugaidi, ukiukaji wa haki za binadamu na kuzusha wasiwasi katika uga wa miradi ya nyuklia ya Iran inayofanyika kwa malengo ya amani.

Katika kipindi hiki pia, tunashuhudia senario mpya ya vyombo vya habari ambavyo vinatoa madai na tuhuma kadha wa kadha dhidi ya Iran ambazo ni za kutunga kupitia ripoti ya jarida la politico.

Katika toleo lake jipya, jarida hilo limenukuu duru za kiintelijensia za Marekani pamoja na maafisa walio karibu na serikali ya nchi hiyo na kuandika kwamba, Iran inapanga njama za kumuua balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini. Mlolongo wa propaganda hizi aghalabu ni zao la vyumba vya kifikra vya Kimarekani-Kizayuni.

Tarehe 11 Oktoba 2011 pia, afisa wa ngazi za juu wa Marekani alitoa madai yasiyo na uthibitisho wowote ule kwamba, Iran ikitumia mamluki ilikuwa ikipanga njama za kumuua balozi wa Saudi Arabia huko Washington. Madai hayo yalikabiliwa na upinzani na malalamiko makubwa ambapo Iran iliuandikia barua Umoja wa Mataifa na kutaka kufuatiliwa madai hayo kupitia vyombo vya kimataifa. Filihali pia, tunashuhudia kwa namna nyingine madai na tuhuma dhidi ya Iran kupitia ripoti ya chombo kimoja cha habari cha Marekani katika kalibu ya madai yaliyopangwa na kuratibiwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwamba, inapanga kutekeleza ugaidi.

Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Kwa hakika madai haya yanatolewa katika hali ambayo, ushahidi na nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa, makundi mengi ya kigaidi yameanzishwa na kulelewa na Marekani. Ushahidi wa wazi kabisa ni kukiri bayana viongozi wa Marekani kwamba, kundi la kigaidi la mtandao wa al-Qaeda na akthari ya makundi ya kigaidi yalianzishwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa minajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yao ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.

Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akitoa radiamali yake kuhusiana na madai hayo amesema: Ni Marekani na serikali ya sasa ya White House ambayo katika miaka ya hivi karibuni imechukua hatua nyingi zisizo na idadi ambazo ziko nje kabisa ya ada za kimataifa kama vile kupanga na kutekeleza makumi ya mipango ya mauaji, uingiliaji wa kijeshi na kiintelijensia, kujitoa katika makubaliano mengi ya kimataifa, kukiuka mamamlaka ya kujitawala mataiafa mengine, kumuua kigaidi Meja Jenerali Qassim Soleimani kamanda wa vita dhidi ya ugaidi na kupuuza kwake misingi ya awali kabisa ya kidiplomasia na hivyo kulibadilisha taifa hilo na kuwa utawala muasi katika uga wa kimataifa.

Meja Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama ilivyotangaza mara chungu nzima ni kuwa, itafuatilia kisheria katika ngazi zote kwenye uga wa kimataifa mauaji ya Meja Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kwamba, haitasemehe hilo na wala katu haitalisahau.

Ripoti ya upotoshaji na yenye malengo maalumu iliyosambazwa na chombo hicho cha habari cha Marekani ina upande mwingine pia ambao unapaswa kutaamaliwa na kuzingatiwa. Tukitupia jicho historia ya huko nyuma tunaona jinsi Washington na baadhi ya miji mikuu ya Ulaya ilivyokuwa ikizusha mambo na kuanzisha anga ya propaganda katika wakati nyeti ikitumia vyombo vya habari kwa ajili ya kuanzisha migogoro bandia kwa minajili ya kufikia malengo ya kisiasa.

Katika wakati huu pia, kwa kuzingatia matukio ya eneo na upinzani unaoongezeka dhidi ya hatua za upande mmoja za Marekani na vilevile hali ya mparaganyiko na ukandamizaji wa umwagaji damu unaofanywa dhidi ya maandamano ya wananchi nchini Marekani yanayolalamikia ubaguzi wa rangi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo, kushuhudiwa harakati na propaganda maalumu za kihabari kwa ajili ya kubadilisha anga ya kisiasa na kuwashughulisha watu na mambo mengine si jambo lililo mbali.

 

Hasa kwa kuzingatia kwamba, historia ya ushindani wa uchaguzi nchini Marekani inaonyesha kuwa, aina hii ya anga hutumiwa kama wenzo wa kampeni za uchaguzi kwa ajili ya kuathiri fikra za waliowengi, hatua ambazo hufanywa na chama tawala.

Kama alivyokumbusha Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii ni kuwa: Upendaji vita wa Marekani katika serikali ya rais wa zamani wa nchi hiyo George W. Bush ulimsukuma awatumie waandishi wa magazeti wanaoamini mambo haraka na hivyo akaanzisha vita dhidi ya Iraq vilivyosababisha hasara kubwa. Hivi sasa pia inaonekana kuna mwelekeo wa kukakariwa hilo ambapo jarida la politico linatumiwa kueneza habari za uongo. Vyombo vya habari vya Marekani vinapaswa kuwa makini visije vikatumiwa na wanasiasa wanaotaka kufikia malengo yao kupitia mgongo wa vyombo hivyo vya habari.