Shughuli za maziko ya shahidi Fakhrizadeh zafanyika mjini Tehran
Shughuli ya maziko ya mwili wa shahid Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran imeanza leo Jumatatu kwa kuchungwa protokali zote za kiafya ili kujiepusha na maambukizi ya corona.
Shughuli hizo zimefanyika katika Wizara ya Ulinzi hapa Tehran na kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa kiserikali na kijeshi wa Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine ameashiria kuweko ishara za wazi kabisa za kuhusika utawala wa Kizayuni wa Israel katika mauaji ya kigaidi ya mwanasayansi mkubwa wa Kiirani wa masuala ya nyuklia na kijeshi na kusema kuwa, mauaji hayo yanaonesha jinsi maadui wanavyopenda vita na jinsi walivyoishiwa.
Dk Mohammad Javad Zarif ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa lugha ya Kifaransa akiashiria jinsi maadui walivyomuua mwanasayansi mkubwa wa Kiirani kwamba, mauji hayo ya kiwogawoga ambayo ndani yake kunaonekana ishara nyingi za wazi za kuhusika Israel, yanaonesha jinsi maadui wanavyopenda vita kutokana na kukata tamaa kwao.
Amesema, Iran inaitaka jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya, ulaani waziwazi ugaidi huo wa kiserikali na uachane na siasa za kindumilakuwili na za nyuso mbili.
Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi Ijumaa jioni katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika viunga vya jiji la Tehran.
Mbali na masuala ya nyuklia na ulinzi, shahidi Fakhrizadeh alikuwa mstari wa mbele pia katika kupambana na ugonjwa wa corona kiasi kwamba, kifaa cha kwanza kabisa cha kuchukulia vipimo vya COVID-19 nchini Iran kilibuniwa na kuundwa na taasisi aliyokuwa akiiongoza yeye.
Salamu za rambirambi zinaendelea kumiminika nchini Iran kutoka kila kona. Miongoni mwa tukio la karibuni kabisa ni hatua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Bw. Badr bin Hamad al Bushaidi, aliyempigia simu waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Iran, Dk Mohammad Javad Zarif kutoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Iran baada ya kuuawa kigaidi, mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran, shahid Mohsen Fakhrizadeh.