Rais wa zamani wa Korea Kusini afungwa maisha jela
-
Rais wa zamani wa Korea Kusini afungwa maisha jela
Mahakama ya Korea Kusini jana Alkhamisi ilimhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo, Yoon Suk Yeol kifungo cha maisha jela kwa kutangaza sheria ya kijeshi mnamo Desemba 2024, na kumtia hatiani mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 65 kwa kuongoza uasi na kuhujumu katiba.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Wilaya ya Kati huko Seoul unaashiria hatua muhimu katika moja ya kesi muhimu zaidi za kisiasa katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo, baada ya vitendo vya Yoon kuitumbukiza Korea Kusini katika mgogoro mkubwa wa kikatiba.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeeleza kuwa, mawakili wa kiongozi huyo wa zamani wa nchi hiyo wanajiandaa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Waendesha mashtaka walikuwa wameomba adhabu ya kifo kwa Yoon — hukumu ya juu zaidi inayotolewa kwa makosa ya uasi na uhaini, chini ya sheria za Korea Kusini.
Maelfu ya wafuasi wa mwanasiasa huyo wa mrengo wa kihafidhina walikusanyika nje ya mahakama jijini Seoul, wakipiga kelele kudai aachiwe huru na wengine wakipeperusha bendera za Marekani wakitumai kuwa Rais Donald Trump angetumia ushawishi wake kushinikiza aachiwe huru.
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, mwaka 2018, Mahakama ya Korea Kusini ilimhukumu kifungo cha miaka 24 jela, aliyekuwa rais wa nchi hiyo Park Geun-hye, baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya ufisadi wa kifedha iliyokuwa ikimkabili.
Park Geun-hye aliuzuliwa madarakani mwishoni mwa mwaka 2016 na baadaye kuzuiliwa, baada ya kupatikana na tuhuma za ufisadi, kutumia vibaya madaraka na kufichua siri za serikali.