Iran yaanza kurutubisha urani kwa asilimia 20 katika kituo cha Fordow
(last modified Mon, 04 Jan 2021 15:46:01 GMT )
Jan 04, 2021 15:46 UTC
  • Iran yaanza kurutubisha urani kwa asilimia 20 katika kituo cha Fordow

Msemaji wa serikali ya Iran ametangaza rasmi habari ya kuanza kurutubishwa tena madini ya urani kwa kiwango cha asilimia 20 katika kituo cha nyuklia cha Fordow, kilichoko kaskazini mashariki mwa mji wa Qum kusini mwa mji mkuu wa nchi hii, Tehran.

Ali Rabiee ametangaza habari hiyo mapema leo na kuongeza kuwa, "Rais (Hassan Rouhani) alitoa agizo katika siku za hivi karibuni la kutekelezwa Sheria ya Hatua ya Kistratajia ya Kuondolewa Vikwazo. Kwa msingi huo, mchakato wa kumimina gesi (katika kituo hicho) umeanza saa chache zilizopita, na sehemu ya kwanza ya urani iliyorutubishwa ya UF6 itapatikana ndani ya saa chache zijazo."

Rabiee ameeleza bayana kuwa, mchakato huo wa kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20 kutoka asilimia 4.6 ya hapo awali ulianza baada ya Iran kuitaarifu rasmi Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Ijumaa iliyopita, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran alisema uamuzi wa kurutubisha urani kwa asilimia 20 unaendana na sheria iliyopasishwa na Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).

Mapema mwezi uliopita wa Disemba, Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) walilitaka Shirika la Atomiki la Iran kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa zaidi ya asilimi 20 kwa ajili ya matumizi ya amani.

Ali Rabiee, msemaji wa serikali ya Iran

Katika kikao cha Disemba Mosi bungeni, wabunge hao waliafiki muswada wa 'Mpango wa Kistratijia wa Kukabiliana na Vikwazo na Kulinda Maslahi ya Taifa'.

Marekani ilijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA mwaka 2015 na kuanza kutekeleza vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatua ambayo iliilazimisha Tehran ianze kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake katika mapatano hayo ya kimataifa.

 

 

Tags