Jeshi la Iran la IRGC lafanya majaribio makubwa ya makombora mapya
(last modified Sat, 16 Jan 2021 07:40:25 GMT )
Jan 16, 2021 07:40 UTC

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) linafanya mazoezi makubwa ya makombora katika jangwa la kati mwa Iran ambapo limefanyia majaribio makombora mapya ya balistiki na ndege za kivita zisizo na rubani.

Awamu ya kwanza ya mazoezi hayo yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu (SAW) 15 ilianza jana Ijumaa ambapo makombora ya balistiki ya kizazi kipya yalivurumishwa mutawalia. Aidha ndege za kivita zisizo na rubani au drone zilitekeleza oparesheni kadhaa katika mazoezi hayo.

Mazoezo hayo yamehudhuriwa na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Meja Jenerali Hossein Salami na Kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC Jenerali Amir-Ali Hajizadeh.

Makombora ambayo yalifanyiwa majaribio katika mazoezi hayo ya Ijumaa ni pamoja na Zulfiqar, Zelzal, na Dezful 

Akizungumza pembizoni mwa mazoezi hayo, Meja Jenerali Salami amesema jeshi la IRGC limepata nguvu mpya kwani silaha hizo zilizofanyiwa majaribio zimeundwa kwa teknolojia ya kisasa kabisa.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilianza mazoezi hayo punde baada ya Jeshi la Majini la Iran kumaliza mazoezi makubwa kusini mwa nchi katika Bahari ya Oman ambapo meli kubwa zaidi ya kivita ya Iran pia ilizinduliwa.

Iran imefanya mazoezi hayo ya kivita huku Marekani ikiwa imekithirisha vitiso vya kijeshi dhidi ya Iran katika siku za mwisho za urais wa Donald Trump.

Mwezi uliopita, Marekani ilituma ndege aina ya B-52 ambayo hutumika kudondosha mabomu ya nyuklia katika eneo la Asia Magharibi kwa lengo la kutoa vitisho dhidi ya Iran.

 

Tags