Iran yasema huenda ikapunguza kiwango cha ushirikiano wake na IAEA
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amesema yumkini Tehran itatazama upya kiwango cha ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Kazem Gharib Abadi amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter Alkhamisi ya jana na kuongeza kuwa, ikilazimu, basi Jamhuri ya Kiislamu itapunguza kiwango cha ushirikiano wake na IAEA.
Kauli ya Gharib Abadi imekuja kufuatia hatua ya utawala mpya wa Marekani kutangaza masharti ya eti kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika ujumbe wake huo, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, ushirikiano na irada njema ni mambo yanayopaswa kutekelezwa na pande mbili husika na wala si suala la upande mmoja.
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amebainisha kuwa, Tehran inatumai kuwa IAEA na pande nyingine husika za JCPOA zitatumia vizuri fursa zilizopewa na Iran, vinginevyo huenda Jamhuri ya Kiislamu ikapunguza kiwango cha ushirikiano kutoka cha juu zaidi hadi cha kawaida.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken siku ya Jumatano katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari aliashiria kadhia ya Iran na kusema: "Iwapo Iran itafungamana kikamilifu na ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, Marekani nayo itafanya hivyo."
Aidha aliongeza kuwa, kurejea Marekani katika JCPOA kutaandamana na kuwepo mapatano madhubuti zaidi na yatakayodumu kwa muda mrefu zaidi yatakayojumuisha masuala mengine yenye utata katika uhusiano na Iran. Amesema mapatano kama hayo yatafikiwa kwa msaada wa waitifaki wa Marekani.