Iran: Ni Marekani ndiyo yenye wajibu wa kurudi kwenye JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, hivi sasa ni Marekani ndiyo yenye wajibu wa kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutekeleza ahadi na majukumu yake.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo mjini Ankara katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na waziri mwenzake wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu wakati akijibu kauli aliyotoa jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken kuhusu kujiunga tena nchi hiyo na JCPOA; na akabainisha kwamba, JCPOA yalikuwa makubaliano ambayo serikali za Marekani, Iran na nchi nyingine tano zilijiunga nayo; na baada ya mazungumzo marefu, nchi hizo zilijadili masuala yote na kisha makubaliano hayo yakaidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Dakta Zarif ameongeza kuwa, makubaliano ya JCPOA yaliandikwa katika anga ya kutoaminiana, kwa hivyo ukabuniwa utaratibu wa kwamba, ikiwa upande mmoja wa makubaliano hautatekeleza majukumu yake, upande mwingine, nao pia utaweza kisheria kuacha kutekeleza majukumu uliyonayo ndani ya makubaliano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na akakumbusha kuwa, Marekani iliamua si tu kujiondoa katika makubaliano, lakini ikawawekea vikwazo na mashinikizo pia wale walioendelea kuheshimu makubaliano hayo; na huo ni mfano dhahiri wa uvunjaji sheria.
Zarif ameeleza kwamba, hatua ilizochukua Iran zimeendana na makubaliano ya JCPOA kwa ajili ya kufidia hatua ilizochukua Marekani; na akafafanua, "hatua ilizochukua Iran hazimaanishi kuwa na makusudio ya kumiliki silaha za nyuklia na tunaitakidi kwamba silaha zote za nyuklia inapasa ziangamizwe na wanaozimiliki, haraka iwezekanavyo."
Dakta Zarif amesisitiza kuwa, punde tu Marekani itakapotekeleza majukumu yake, na Iran ikashuhudia manufaa inayopata kwa kutekelezwa majukumu hayo, nayo pia itatekeleza kikamilifu majukumu yake na kwamba msimamo huo umetangazwa katika ngazi ya juu kabisa ya Jamhuri ya Kiislamu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.../