Luteka ya 'Mtume Mtukufu 16' yaanza kusini mwa Iran
Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kinatazamiwa kuanza mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu 16 katika maeneo ya kusini magharibi mwa Iran.
Vikosi mbalimbali vya IRGC vinatazamiwa kushiriki katika luteka hiyo. Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha SEPAH, Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema hii itakuwa awamu ya mwisho wa maneva ya Mtume Mtukufu 16.
Jenerali Pakpour amesema mazoezi hayo ya kijeshi yatahusisha kikosi cha ndege za kivita zisizo na rubani (droni), vifaru, kikosi cha anga, vikosi maalumu n.k.
Amesema lengo la mazoezi hayo mbali na kutathmini mafanikio ya Iran katika uga wa ulinzi na kujihami kwa mnasaba wa miaka 42 ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini pia yatatuma ujumbe kwamba vikosi vyote vya nchi hii viko macho na vimejiandaa kukabiliana na vitisho na chokochoko za maadui.
Januari 15, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilifanya awamu ya kwanza ya mazoezi hayo yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu (SAW) 15.
Katika mazoezi hayo makubwa yaliyofanyika katika jangwa la kati mwa Iran, Jamhuri ya Kiislamu ilifanyia majaribio makombora mapya ya balistiki na ndege za kivita zisizo na rubani.