Neematzadeh: Marekani ndio inayokwamisha Iran kujiunga na WTO
Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran amesema tatizo la Iran kujiunga na Shirika la Biashara Duniani (WTO) ni la kisiasa na linatokana na upinzani wa Marekani.
Mohammad Reza Neematzadeh, ameyasema hayo kwenye kongamano la "Mwenendo wa Utungaji Sheria; Yanayolazimu na Njia za Ufumbuzi", ambalo limehudhuriwa na wabunge wateule wa Majlisi ya 10 ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Amesema sababu kuu ya kutojiunga Iran na Shirika la Biashara Duniani si ya kiufundi bali ni ya kisiasa, kwa sababu wakati suala hilo lililpowasilishwa, Marekani ililipinga.
Neematzadeh ameashiria mazungumzo mapana na ya kina iliyofanya Iran na Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani, Umoja wa Ulaya na nchi nyengine nyingi hasa baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia (JCPOA) na kubainisha kuwa hata nchi nyingi zimewasiliana na Marekani kuitaka iache kukwamisha kujiunga Iran na shirika hilo.
Akihutubia kongamano hilo, Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Iran Mohsen Jalalpur amesema ili kujiunga na Shirika la Biashara Duniani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaufanya uchumi wake kuwa wa ushindani na kupiga hatua kuelekea soko huru.
Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Iran amefafanua kuwa sera kuu za Uchumi wa Muqawama zina maana ya kujitokeza kwa kiwango cha juu kabisa taifa la Iran katika uga wa uchumi kwa kutegemea zaidi ndani ya nchi na kuzingatia pia nje ya nchi.../