Chanjo ya COVID-19 ya Iran ya Fakhra yaanza kufanyiwa majaribio + Video
Awamu ya kwanza ya majaribio kwa mwanadamu ya chanjo ya COVID-19 ya Fakhra iliyotegenezwa Iran imeanza leo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, Ahmad Karimi, Mkurugenzi wa Mradi wa Chanjo ya Fakhra ameshiriki katika uzinduzi wa majaribio hayo Jumanne na kusema: "Mchakato wa utafiti wa chanjo hii ya COVID-19 ulianza miezi kadhaa iliyopita."
Amesema chanjo hii imepita majaribio kwa wanyama na haikuwa na madhara yoyote na sasa imeingia katika awamu ya kwanza ya majaribio kwa mwanadamu.
Mtu wa kwanza kudungwa chanjo hiyo ya Fakhra ni mwanae Shahidi Mohsen Fakhrizadeh mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya kijeshi wa Iran aliyeuawa na magaidi mwezi Novemba mwaka jana.
Karami amesema kiwanda cha kuzalisha chanjo hiyo kwa wingi tayari kimeshajengwa na inatazamiwa kuanza kutumiwa katika msimu wa joto.
Chanjo hiyo imeundwa na Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran. Shirika hilo lilikuwa likisimamiwa na Shahidi Fakhrizadeh hadi wakati alipouawa shahidi.