Rais Rouhani: Endapo Marekani itatekeleza ahadi zake, sisi pia tutafanya hivyo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, endapo kutakuwa na azma imara na Marekani ikarejea katika mazingira ya kabla ya vikwazo, sisi pia siku hiyo hiyo tutaanza kutekeleza ahadi zetu.
Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika kikao na baraza lake mawaziri ambapo pamoja na kubainisha kwamba, vikwazo ni dhulma kubwa dhidi ya taifa la Iran na vinapaswa kuondolewa ameeleza kwamba, endapo kutakuwa na azma thabiti na ya kweli, na Marekani ikarejea katika mazingira ya kabla ya vikwazo, basi sisi pia siku hiyo hiyo tutaanza kutekeleza ahadi zetu.
Rais Rouhani sambamba na kueleza kuwa, Marekani ndio mhusika mkuu wa asilimia mia kwa mia katika suala la vikwazo na kwamba, hilo halina shaka amesema bayana kuwa, katika kipindi cha utawala wa Donald Trump Marekani ilikiuka sheria, ilikanyaga utu na ubinadamu, ilifanya ugaidi na ikawawekea vikwazo vya kila kitu wananchi wetu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya iran amebainisha kuwa, Marekani isiyo na utu imewawekea vikwazo wananchi wa Iran hata katika uga wa dawa na chakula.

Amesema pia kuwa, serikali iliyopita ya Marekani ndio utawala khabithi zaidi katika historia ya Marekani kwa eneo la Asia Magharibi, Iran, taifa la Palestina na hata kwa wananchi wenyewe wa taifa hilo la kibeberu.
Rais Rouhani ameihutubu serikali mpya ya Marekani kwa kusema, nyinyi ndio mnaoendelea kufanya ugaidi, mumezuia fedha zetu na hamruhusu zitufikie, mnakwamisha biashara zetu na hata mnafanya njama kuhakikisha kwamba, hatupati hata chanjo ya Corona.