Zarif: Hakuna udharura wa kufanyika mkutano kati ya Iran na Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani juu ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwamba hakuna udharura wa kufanyika mkutano baina Tehran na Washington.
Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, muda mfupi baada ya kufanyika kikao cha Kamati ya Pamoja ya JCPOA kwa njia ya inatenti.
Dakta Zarif ameashiria mkutano huo wa 18 wa hapo jana uliowaleta pamoja wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, China, Ufaransa, Ujerumani, Russia, Uingereza na Iran na kubainisha kuwa: Katika mkutano wa mawasiliano ya video wa Kamati ya Pamoja, Iran, EU/E3+2 zimekubaliana kufanya mkutano mwingine wa ana kwa ana Jumanne mjini Vienna. Lengo ni kuhitimisha haraka mchakato wa kuiondolea Iran vikwazo vyote, mkabala wa Iran kusimamisha hatua za kupunguza uwajibikaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Hakuna mkutano baina ya Iran na Marekani, hilo halina udharura wowote.
Hapo jana, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ambaye aliiwakilisha Iran katika kikao cha jana, alisema baada ya mkutano huo kuwa, kuondolewa vikwazo na Marekani ndiyo hatua ya kwanza ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.