Rouhani: JCPOA imeipa uhalali sekta ya nyuklia ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kupasishwa kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA kuliipa uhalali kamili wa kisheria sekta ya nyuklia ya taifa hili.
Rais Rouhani amesema hayo leo kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa, miradi ya nyuklia ya nchi hii inafanyika kwa malengo ya amani na kiraia.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa, nchi za Magharibi zilikuwa na wasiwasi wa bure juu ya miradi ya nyuklia ya taifa hili, lakini mapatano ya JCPOA yalikuwa kuthibitisha kuwa miradi hiyo inatumika katika masuala ya amani kama sekta ya viwanda, kilimo, tiba, nishati na umeme.
Ameongeza kuwa, Wamagharibi walilihangaisha taifa la Iran kwa muda wa miaka 16, kwa kutumia kisingizio cha kutiwa wasiwasi na miradi ya nyuklia ya nchi hii yenye malengo ya amani.
Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, kwa kusaini makubaliano ya JCPOA, Iran ilibadilisha propaganda na mtazamo potufu kuwa miradi yake ya nyuklia ni haramu na kwa kufanya hivyo, Tehran iliweza kutengua maazimio yote ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kulaani miradi hiyo.

Amekumbusha kuwa, athari na makovu ya kitendo cha Marekani cha kuishambulia Japan kwa silaha za nyuklia katika Vita vya Pili ya Dunia yangali yanahisika hadi hii leo.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, Iran tangu hapo mwanzo iliionesha dunia kuwa miradi yake haina malengo ya kijeshi, kwa kusani mkataba unaopiga marufuku uzalishaji na uenezaji wa silaha za nyuklia (NPT).