Rouhani: Iran inapanga kuzindua mchakato mpana wa chanjo ya COVID-19
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i69246-rouhani_iran_inapanga_kuzindua_mchakato_mpana_wa_chanjo_ya_covid_19
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali ina mpango wa kuzindua mpango mkubwa wa chanjo ya COVID-19 au corona ili kulinda afya ya watu wote.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 20, 2021 10:42 UTC
  • Rouhani: Iran inapanga kuzindua mchakato mpana wa chanjo ya COVID-19

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema serikali ina mpango wa kuzindua mpango mkubwa wa chanjo ya COVID-19 au corona ili kulinda afya ya watu wote.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika 'Kikao cha 19 cha Uratibu wa Masuala ya Kiuchumi Serikalini' na kuongeza kuwa, pamoja na kuwepo mashinikizo na matatizo mengi katika kupata fedha kutokana na vita vya kiuchumi vya adui na vikwazo vyake vilivyo dhidi ya ubinadamu, sekta mbali mbali za serikali zimejitahidi kukidhi mahitaji ya chanjo. Amesema jitihada hizo za Iran zinafanyika pamoja na kuwepo uhaba mkubwa wa chanjo ya corona duniani kutokana mahitajio makubwa ya chanjo katika nchi zote.

Rouhani pia amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, adui amekuwa akifuatilia vita vya kiuchumi dhidi ya Iran ili kuibua janga la njaa nchini lakini serikali imeweza kuhakikisha kuwa wananchi wanapata bidhaa zote wanazohitaji na hivyo adui hakuweza kufikia malengo yake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria nafasi muhimu ya viwanda nchini katika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya wananchi na kuongoza kuwa: 'Bidhaa za dharura ambazo watu wanazihitajia zinapaswa kuruhusiwa kuingia nchini bila kucheleweshwa katika idara za forodha."