'Madai ya Saudia dhidi ya Iran ni kichekesho'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i7006-'madai_ya_saudia_dhidi_ya_iran_ni_kichekesho'
Ofisi ya Uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imepinga tuhuma za mwakilishi wa Saudi Arabia katika umoja huo dhidi ya Iran na kuzitaja kuwa kichekesho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 13, 2016 23:11 UTC
  • 'Madai ya Saudia dhidi ya Iran ni kichekesho'

Ofisi ya Uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imepinga tuhuma za mwakilishi wa Saudi Arabia katika umoja huo dhidi ya Iran na kuzitaja kuwa kichekesho.

Jawad Safai, mwambata wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema inafahamika wazi kuwa Saudia inachochea na kuhimiza malumbano ya kimadhehebu.

Safai alikuwa akijibu tuhuma zilizotolewa na balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran katika kikao ambacho kiliitishwa kujadili mada ya 'Itikadi za Kigaidi'. Kikao hicho kiliitishwa kufuatia pendekezo la Misri ambayo ni mwanachama wa kiduru wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Safai amesema ni jambo la kushangaza kuona Saudia ikiituhumu Iran kuwa eti inachochea malumbano ya kimadhehebu wakati ambao kila mtu anafahamu chimbuko la makundi ya wakufurishaji liko wapi.

Ameongeza kuwa watawala wa Saudia na wahubiri wa kidini nchini humo wanachochea taasubi za kimadhehebu na kwamba jambo hilo liko wazi na halihitaji ufafanuzi. Huku akiyataja madai ya Saudia dhidi ya Iran kuwa yasiyo na msingi, mwanadiplomasia huyo wa Iran ameashiria hotuba ya Imamu wa Msikiti Mkuu wa Makkah, ambaye huteuliwa na Saudia. Katika hotuba yake ya kichochezi hivi karibuni, Imamu huyo alisema na hapa tunanukuu: "Natangaza kwa sauti kubwa kuwa vita vyetu na Iran ni vita vya Sunni na Shia. Hataka kama vita hivi si vya kimadhehebu tutavifanya viwe vya kimadhehebu. Uhasama wetu na Mashia Utaendelea daima." Mwisho wa kunukuu.

Safai amesema matamshi hayo ni ishara ya wazi kuhusu ni kina nani wanaoeneza fikra za ukufurishaji kwa lengo la kuwaangamiza wengine. Aidha amesema balozi wa Saudia ambaye ana mitazamao sawa na mwakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel anapaswa kufahamu kuwa Hizbullah ya Lebanon si kundi la kigaidi kama alivyodai bali ni sehemu ya muundo rasmi wa serikali ya Lebanon.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema hatua ya nchi ya Kiislamu (Saudia) kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuihujumu Hizbullah ni jambo ambalo linatoa pigo kwa Ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu kote duniani.