Iran yalaani kitendo cha Canada kuzuia Wairani nchini humo kupiga kura uchaguzi wa rais
(last modified Fri, 11 Jun 2021 12:35:01 GMT )
Jun 11, 2021 12:35 UTC
  • Iran yalaani kitendo cha Canada kuzuia Wairani nchini humo kupiga kura uchaguzi wa rais

Msemaji wa Tume ya Uchaguzi ya Iran amesema hatua ya Canada ya kukataa kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Wairani wanaoishi Canada wanapiga kura katika uchaguzi wa rais wa Iran, ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Taarifa iyotolewa na Sayyid Ismail Mousavi, Msemaji wa Tume ya Uchaguzi ya Iran imesema, serikali ya Canada imekataa kutoa ushirikiano ili kuwezesha kufanyika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndani ya ardhi ya nchi hiyo ya Amerika Kaskazini ambayo ina idadi kubwa ya wahajiri Wairani. Ameongeza kuwa kadhia hii inafuatiliwa kwa karibu na balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York ambaye atawasiliana na balozi wa Canada katika umoja huo.

Inafaa kuashirikia hapa kuwa, Iran na Canada hazina uhusiano wa kidiplomasia.

Mousavi ameongeza kuwa: 'Bado hatujapokea jibu kutoka serikali ya Canada kuhusu kufanyika moja kwa moja uchaguzi wa rais wa Iran katika ardhi ya Canada."

Msemaji wa Tume ya Uchaguzi ya Iran amesema, kwa kuzingatia muda mchacho uliobakia kabla ya kufanyika uchaguzi, ni vigumu sasa kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kutuma wasimamizi wa uchaguzi nchini humo, na kwa hivyo kwa sasa haiwezekani kufanya uchaguzi moja kwa moja.

Amesema kwa kuzingatia mipango iliyofanywa, Ofisi ya Kulinda Maslahi ya Iran mjini Washington itaandaa zoezi hilo la kupiga kura ambapo Wairani waishio Canada watafika katika moja ya miji ya mipakani ya Marekan kupiga kura.

Wagombea urais nchini Iran

Wakati huo huo, Ubalozi wa Iran nchini Uingereza umesema wananchi wa Iran walioko katika nchi hiyo ya bara Ulaya watakuwa na fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu katika mji mkuu London, na miji mingine sita mikubwa ya nchi hiyo.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya wiki ijayo ya tarehe 18 mwezi huu wa Juni, 2021 ndani na nje ya nchi. Wagombea urais katika uchaguzi huo ni Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi, Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.

Rais wa sasa Hassan Rouhani anayemaliza muhula wake wa pili mfululizo haruhusiwi kugombea urais katika awamu hii.

Wagombea hao wa Urais wanaendelea kunadi sera zao katika majukwaa mbalimbali, na kesho Jumamosi wanatazamiwa kushiriki katika mdahalo wa tatu na wa mwisho wa urais.