Luteka ya Walinzi wa Anga ya Velayat-1400 yaanza nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i75668-luteka_ya_walinzi_wa_anga_ya_velayat_1400_yaanza_nchini_iran
Vikosi vya Anga vya Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran vimeanza mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la 'Walinzi wa Anga ya Velayat-1400' katika maeneo ya jangwani ya katikati mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2021 04:41 UTC
  • Luteka ya Walinzi wa Anga ya Velayat-1400 yaanza nchini Iran

Vikosi vya Anga vya Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran vimeanza mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la 'Walinzi wa Anga ya Velayat-1400' katika maeneo ya jangwani ya katikati mwa nchi.

Brigedia Jenerali Ghader Rahimzadeh, Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Khatam al-Anbia ametangaza habari ya kuanza mazoezi hayo ya pamoja leo Jumanne katikati mwa Iran.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, vikosi vinavyoshiriki kwenye luteka hiyo ya kijeshi ni pamoja na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran, kitengo cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) na Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Brigedia Jenerali Ghader Rahimzadeh, Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Khatam al-Anbia 

Amesema mfumo wa Kamandi na Udhibiti wa Eneo (ROC) wa IRGC, na mifumo ya rada ya Meraj, Fatah-2, Bashir na Quds iliyotengenezewa na wataalamu wa humu nchini, sanjari na aina kadhaa za droni (ndege zisizo na rubani) ni miongoni mwa suhula na zana za kivita zitakazotumika kwenye maneva hayo.

Brigedia Jenerali Rahimzadeh amesisitiza kuwa, lengo la mazoezi hayo ya kijeshi ni kunyanua juu uwezo na utayarifu wa jeshi la Iran kwa kushirikisha vikosi vya Jeshi la Anga na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SEPAH) katika mazingira yanayokaribiana sana na ya vita halisi.

Mazoezi haya ya kijeshi yanafanyika kwa kutegemea utaalamu wa wasomi wa ndani ya nchi katika kudhamini mahitaji ya kiulinz, kwa shabaha ya kujiweka tayari kuzuia hujuma ya aina yoyote ya mabeberu wa kimataifa.