Saeed Khatibzadeh: Iran inafuatilia kwa makini matukio ya Sudan
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubainisha matukio ya kutia shaka ya hivi karibuni nchini Sudan hayasaidii mchakato wa demokrasia katika nchi hiyo kusema kuwa, Tehran inafuatilia kwa umakini matukio hayo.
Saeed Khatibzadeh amebainisha kuwa, kuondoa kwa njia isiyo ya kidemokrasia moja ya taasisi ya utawala ni kupuuza matakwa ya wananchi na hatua hiyo haitadhamini malengo yanayofuatiliwa na wananchi wa nchi hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, kumeonekana ishara za kuweko mkono na uingiliaji wa kigeni uliokuwa na taathira katika matukio hayo ya Sudan na kusisitiza kwamba, mirengo ya Kizayuni haijaficha furaha yao kwa yale yaliyotokea nchini Sudan.
Aidha amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kusisitizia udharura wa kuwa macho watawala wa Sudan inazitaka pande zote za ndani nchini humo kufanya mazungumzo jumuishi ya mirengo yote ya Sudan.
Ripoti zinasema kwa akali watu wanane wameuawa na wengine 170 wamejeruhiwa katika maandamano yanayofanyika nchini Sudan tangu jeshi liliponyakua madaraka ya nchi mapema wiki hii.
Siku ya Jumatatu, Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, ambaye anaonekana kuwa ndiye kiongozi wa Sudan tangu aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir alipong'olewa madarakani kupitia maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana, aliivunja serikali inayoongozwa na raia na kuamuru kukamatwa na kuwekwa kizuizini maafisa kadhaa wa ngazi ya juu wa serikali hiyo, hatua ambayo sasa imeitumbukiza Sudan katika vurufu, machafuko na maandamano.