Waziri: Mafanikio ya mazungumzo ya Vienna yanategemea kuondolewa vikwazo vyote Iran
(last modified Tue, 09 Nov 2021 08:19:43 GMT )
Nov 09, 2021 08:19 UTC
  • Waziri: Mafanikio ya mazungumzo ya Vienna yanategemea kuondolewa vikwazo vyote Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kufanikiwa mazungumzo ya mjini Vienna, Austria kuhusu makubaliano ya JCPOA kutategemea na kuondolewa vikwazo vyote Iran, sambamba na kuifanya ya kawaida miamala ya kibiashara na Tehran.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Uingereza, Liz Truss na kuongeza kuwa, mazungumzo hayo ya kujaribu kuhuisha utekelezaji wa JCPOA yatazaa matunda iwapo pande zote husika zitarejea katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza bayana kuwa, sharti Iran ipate dhamana ya kutekelezwa kivitendo nukta zote zitakazoafikiwa kwenye mazungumzo hayo yanayotazamiwa kuanza tena mwishoni mwa mwezi huu.

Kadhalika Amir-Abdollahian ameitaka serikali ya Uingereza kuilipa Jamhuri ya Kiislamu deni lake la huko nyuma haraka iwezekanavyo, kwani hiyo ya haki ya msingi ya taifa la Iran.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz Truss amesema nchi hiyo ya Ulaya pamoja na Ujerumani na Ufaransa zina hamu ya kuona mazungumzo hayo ya Vienna yanapiga hatua na hayasuisui tena.

Vikao vya Vienna tena mwishoni mwa Novemba

Hapo awali,  Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya mazungumzo pia na mwenzake wa Ujerumani, ambapo amesisitizia udharura wa kuondolewa Tehran vikwazo vyote haramu mara moja.

Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa upande wake amedai kuwa, dhamira kuu ya nchi hiyo ya Ulaya ni kuona pande zote husika zinarejea mara moja kwenye makubaliano ya JCPOA, na zinatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Tags