Raisi: Nabii Isa AS, nembo ya muqawama dhidi ya madhalimu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtaja Nabii Isa Masih (AS) kuwa ni nembo ya mapambano dhidi ya madhalimu.
Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo katika ujumbe aliowatumia viongozi wa ulimwengu wa Kikristo, kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuwadia mwaka mpya wa Miladia wa 2022.
Sambamba na kuwapongeza Wakristo kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Miladia ulioanza leo Jumamosi, Rais Raisi amebainisha kuwa, Nabii Isa (AS) ni Mtume wa ustahamilivu na amani, na pia ni shakhsia anayeheshimiwa na kuenziwa mno na Waislamu.
Rais wa Iran ameeleza kuwa, Nabii Isa AS mbali na kuwa shina la muqawama dhidi ya madhalimu, lakini pia ni Mtume anayewapa Ilhamu na motisha wanaopigania haki duniani dhidi ya madikteta.
Sayyid Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, ushirikiano miongoni mwa mataifa ya dunia mkabala wa mgogoro wa kiafya unaoshuhudiwa duniani, hususan katika uga wa ugavi wa chanjo; pamoja na kwamba baadhi ya nchi zinakwamisha mpango huo kutokana na vikwazo; lakini unaashiria wazi haja ya kuwa na mfumo wa kimataifa ambao unaweza kudhamini mantiki, haki na umaanawi.
Ametamatisha ujumbe wake kwa kusema kuwa, anatumai changamoto zinazoikabili jamii ya mwanadamu zitapatiwa ufumbuzi, kwa kutegemea maadili ya kiakhlaqi za dini za Ibrahim AS, na kama pia alivyoahidi Nabii Isa Masih, na kutiliwa mkazo na kitabu cha Injili.