Uzayuni hauna nafasi yoyote katika mustakbali wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78870-uzayuni_hauna_nafasi_yoyote_katika_mustakbali_wa_dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu upayukaji wa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, Tehran iko imara katika kulinda maslahi yake ya kitaifa na kwamba, Uzayuni hauna nafasi katika mustakbali wa dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2022 23:19 UTC
  • Uzayuni hauna nafasi yoyote katika mustakbali wa dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu upayukaji wa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, Tehran iko imara katika kulinda maslahi yake ya kitaifa na kwamba, Uzayuni hauna nafasi katika mustakbali wa dunia.

Ijapokuwa majibu hayo ya Hossein Amir-Abdollahian ni mafupi lakini yana maana pana sana. Viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakijiliwaza kwa kupayuka maneno chapwa yasiyo na msingi. 

Ikiwa ni kuendeleza bwabwaja hizo, Yair Lapid, waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni amedai kuwa, utawala huo eti unaweza kuishambulia Iran bila ya hata kuijulisha Marekani kwani eti utawala huo hauna haja ya kupata idhini ya yeyote katika kulinda usalama wake.

Amedai kuwa, ingawa anapendelea kuona kunachukuliwa hatua za kimataifa dhidi ya mradi wa nyuklia wa Iran, lakini kama itabidi, basi utawala wa Kizayuni hautapoteza fursa yoyote utakayoipata.

Lakini swali la kwanza kabisa linalojitokeza hapa kuhusu upayukaji wa maneno chapwa ya waziri huyo wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni ni kwamba lengo la kiongozi huyo wa utawala wa Kizayuni ni lipi hasa? Majibu ni kwamba, bwabwaja za viongozi wa Israel hazitoki kwenye malengo mawili makuu.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Lengo la kwanza ni kushindwa Wazayuni kuficha wahka na wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa Marekani kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA uwezekano ambao umezidi kupata nguvu baada ya kuanza mazungumzo ya Vienna yanayojadili njia za kuondolewa Iran vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa na Marekani. Lakini inaonekana wazi kwamba, wasiwasi huo wa Wazayuni hauishii tu kwenye uwezekano wa kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA bali woga mkubwa wa Wazayuni ni kusambaratika na kufutika utawala huo pandikizi katika uso wa dunia. Ili kujiepusha na janga hilo, utawala wa Kizayuni unahitajia msaada wa kila upande wa Washington hususan kupitia siasa za kuzusha migogoro katika eneo la Asia Magharibi. Kuongezeka bwabwaja za viongozi wa utawala wa Kizayuni kunaakisi wahka na woga huo. 

Wimbi jipya la upayukaji wa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel lilianza wakati yalipokaribia mazungumzo juu ya namna ya kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA tarehe 29 Novemba 2021. Tangu wakati huo hadi hivi sasa viongozi hao wa Israel wamekuwa wakitoa vitisho hivi na vile dhidi ya Tehran wakidai kuwa eti wana uwezo wa kushambulia maeneo ya nyuklia ya Iran.

Hata hivyo, Ehud Olmert, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni alifichua kuwa, utawala huo hauna nia ya kuishambulia Iran na kwamba maneva na mazoezi yake yote ya kijeshi ni kwa lengo la kuitishia Marekani tu, na hayailengi Iran

Bendera ya utawala wa Kizayuni

 

Amma lengo la pili la bwabwaja za viongozi wa Israel ni kuendelea na propaganda zao za uongo kuhusu mradi wa nyuklia wa Tehran na kujaribu kuonesha kuwa mradi huo ni hatari kwa usalama wa dunia. Vile vile ni vyema tukasema hapa kuwa, malengo yote hayo mawili yana mfungamano wa karibu na njama za Israel za kufanikisha malengo yake haramu katika eneo hili.

Hata hivyo siasa hizo si mara zote zinakuwa ni kwa faida ya Marekani na Ulaya. Paul R. Pillar, afisa wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi wa masuala ya kimataifa ameandika makala chini ya kichwa cha maneno: "Madai ya kila siku ya Israel kuhusu kuishambulia Iran, yanahatarisha manufaa ya Marekani" na ndani yake ametahadharisha kuhusu madhara inayopata Marekani kwa kufuata kwake maneno ya viongozi wa Israel kuhusu Iran.

Kiujumla ni kwamba madai yanayotolewa na viongozi wa utawala wa Kizayuni kuhusu Iran yamejaa uongo na uzushi. Lengo jingine kuu la viongozi wa utawala huo pandikizi ni kuficha hatari za silaha zake za nyuklia katika eneo hili na duniani kwa ujumla. Jinai za utawala wa Kizayuni ni kubwa sana dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina na kama eneo hili litaishi kwa utulivu, dunia itaelekeza nguvu zake katika kupambana na jinai hizo za Wazayuni na hilo ni lengo jengine la viongozi wa Israel la kueneza maneno ya uongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili utawala wa Kizayuni uweze kuficha jinai zake mbele ya walimwengu. Vile vile viongozi wa Israel wanataka kuvuruga uhusiano wowote ule wa Iran na nchi nyingine hasa majirani zake lakini uhakika utabakia kuwa ule ule uliobainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwamba, Uzayuni hauna nafasi katika mustakbali wa dunia.