Jan 29, 2022 13:16 UTC
  • Iran, makundi ya Iraq yalaani shambulizi dhidi ya uwanja wa ndege wa Baghdad

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi maarufu ya Iraq yamelaani shambulizi la hivi karibuni la roketi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, wakisema hatua hizo za "kutiliwa shaka" zinalenga kuyumbisha usalama wa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh amesema: "Vitendo kama hivyo vinavyotiliwa shaka vinasababisha ukosefu wa usalama na machafuko nchini Iraq na vinafungua njia kwa wafitini na watu wasiolitakia mema taifa la Iraq kuathiri huduma zinazotolewa na serikali kwa raia wa Iraq."

Khatibzadeh amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa  ikiunga mkono juhudi za kuimarisha usalama na amani nchini Iraq, maendeleo ya ustawi wa nchi hiyo na juhudi za serikali za kuimarisha usalama.

Saeed Khatibzadeh

Wakati huo huo Abu Ali al-Askari, afisa wa usalama wa kundi la Kata'ib Hezbullah amesema, sera ya kuvuruga usalama ya walaghai na mafisadi haina faida yoyote, na amewataka maafisa wa usalama na vikosi vya PMU kuwasaka mamluki na wafuasi wao waliohusika na hujuma hiyo.

Harakati ya Hashd al-Sha'abi (PMU) ilikuwa na nafasi muhimu katika kulifurusha kundi la Daesh na magenge mengine ya kigaidi katika ardhi ya Iraq.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Iraq, roketi sita zilishambulia uwanja wa ndege wa Baghdad mapema siku ya Ijumaa, na kuharibu ndege mbili za kibiashara, lakini hakuna mtu aliyeuawa au kujeruhiwa. 

Ripoti zinasema jumla ya roketi 10 zilirushwa wakati wa shambulio hilo. Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo. 

Tags