Oct 13, 2023 11:37 UTC
  • Safari ya kieneo ya Amir Abdollahian inayoangazia vita vya Gaza

Huku utawala wa Kizayuni ukiendeleza hujuma na vita vyake vya jinai dhidi ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza, Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasisitiza ulazima wa kukomeshwa jinai hizo za Wazayuni kwa kufanya safari katika nchi kadhaa za eneo.

Hossein Amirabdollahian alisafiri Iraq tarehe 12 Oktoba ambapo alikutana na kushauriana na waziri mkuu wa nchi hiyo pamoja na mshauri wa usalama wa taifa. Amir Abdollahian, akiwa katika sehemu ya pili ya safari yake katika eneo baada ya Baghdad, amewasili mjini Beirut Lebanon leo Ijumaa asubuhi akiongoza ujumbe wa ngazi za juu ambapo amekutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Miqati, Waziri wa Mambo ya Nje Abdallah Bohamid na Seyyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon. Inatazamiwa kuwa Amir Abdollahian ataelekea Damascus, Syria baada ya Beirut.

Kuchunguzwa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza ndio lengo kuu la mashauriano ya Amir Abdollahian na viongozi wa Iraq na Lebanon. Katika mashauriano hayo, pande hizo zimejadili masuala kadhaa na kueleza mtazamo mmoja kuhusu vita dhidi ya Gaza.

Suala la kwanza ni kwamba kile kinachofanywa na utawala unaoukalia kwa mabavu Quds Tukufu dhidi ya Ukanda wa Gaza ni mfano wa wazi wa uhalifu wa kivita. Katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza, takriban Waislamu 1,600 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 7,600 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), takriban wahanga 450 kati ya waliouawa shahidi ni watoto. Aidha, kutokana na hatua ya utawala huo wa kibaguzi kukata umeme na maji, vituo vya matibabu haviwezi tena kutoa huduma za dharura, na sasa Gaza inakabiliwa na hali mbaya na hatari mno. Kwa kuzingatia hayo, Hossein Amirabdollahian amesisitiza katika kikao na viongozi wa Iraq kwamba, mambo yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza ni mfano wa wazi wa jinai za kivita. Mtazamo huo pia umesisitizwa na viongozi wa Iraq.

Jinai za kivita za Israel katika Ukanda wa Gaza

Mhimili wa pili wa mashauriano hayo ni kwamba juhudi za kieneo na kimataifa za kukomesha vita dhidi ya Ukanda wa Gaza zinapaswa kuongezeka kwa ajili ya kuzuia vita vya Gaza kugeuka kuwa vita vya kieneo. Utawala huo ambao karibuni ulikabiliwa na pigo kubwa zaidi la kijeshi katika historia yake ya miaka 75 kupitia Kimbunga cha al-Aqsa, unajaribu kuanzisha vita vya nchi kavu dhidi ya Gaza na kuunda mistari mipya ya vita dhidi ya Lebanon na Syria.

Iwapo utawala wa Kizayuni utafanya makosa hayo ya kistratijia, vita vya Gaza vitageuka na kuwa vita vya kieneo. Kuhusiana na suala hilo, Najib Miqati, Waziri Mkuu wa Lebanon katika kikao chake na Amir Abdollahian amesema kuwa mawasiliano ya kidiplomasia ni muhimu sana katika kudhibiti hali hiyo na kutaja nafasi ya Iran katika juhudi hizo za kidiplomasia kuwa muhimu. Amesisitiza kuwa juhudi zote zinapaswa kufanywa kwa shabaha ya kuzuia kutokea vita vya kieneo.

Mhimili wa tatu katika mashauriano ya Amir Abdollahian na viongozi wa Iraq na Lebanon umeangazia kukosolewa siasa na tabia ya Marekani katika vita hivyo. Huku ikiilaani Hamas na kuiweka harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina katika orodha ya makundi ya kigaidi sawa na Daesh, serikali ya Marekani imetoa msaada na uungaji mkono mkubwa kwa utawala ghasibu wa Israel. Katika kikao na Najib Mikati, Hossein Amirabdollahian ameashiria kwamba uungaji mkono usio na kikomo wala masharti wa Marekani kwa jinai za Israel utafanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi, na kusema kwamba Marekani inamtaka kila mtu ajizuie kuchukua hatua zaidi za vita, lakini yenyewe inatoa silaha kwa Israel na kuusaidia utawala huo kwa hali na mali.

Tags