Khatibzadeh: Uhai wa utawala vamizi wa Quds unafungamana na kufanya mauaji
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhai wa utawala vamizi wa Quds unafungamana na ukandamizaji na kufanya mauaji.
Saeed Khatibzadeh amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo akiashiria safari ya hivi karibuni ya Rais wa utawala ghasibu wa Israel katika Umoja wa Falme za Kiarabu ameeleza kwamba, utawala bandia na unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu ni utawala unaoanzisha migogoro na unaofuatilia siasa za kibaguzi (apartheid).
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel ni doa jeusi kwa jamii ya mwanadamu na umekuwa ukifanya njama za kuhamishia migogoro yake katika ardhi nyingine.
Saeed Khatibzadeh amezungumzia kusimamishwa kwa muda mazungumzo ya nyuklia ya Vienna na kubainisha kwamba, katika kipindi cha majuma matatu ya mazungumzo hayo, kumepigwa hatua kubwa na muhimu.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kama pande zingine hususan Marekani itaheshimu na kuzingatia matakwa ya haki ya Iran na kutotaka kitu zaidi yaliyoko katika makubaliano hayo bila shaka itawezekana kufikiwa makubaliano ya kudumu.
Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekaribisha kustawishwa uhusiano wa Tehran na nchi za eneo ikiwemo Iraq na Saudi Arabia na kusema kwamba, kadiri kutakapokuweko misimamo ya pamoja ndivyo kunavyopatikana fursa zaidi za ushirikiano.