Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; Marekani dhihirisho la “Ujahilia wa Kisasa”
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80934-mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu_marekani_dhihirisho_la_ujahilia_wa_kisasa
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uchafu mwingi wa kimaadili uliokuwa katika zama za ujahilia unashuhudiwa hii leo kwa sura pana, kubwa na ya kuratibiwa katika ulimwengu wa Magharibi unaojulikana kama uliostaarabika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2022 09:26 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu; Marekani dhihirisho la “Ujahilia wa Kisasa”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uchafu mwingi wa kimaadili uliokuwa katika zama za ujahilia unashuhudiwa hii leo kwa sura pana, kubwa na ya kuratibiwa katika ulimwengu wa Magharibi unaojulikana kama uliostaarabika.

Ayatullah Ali Khamenei alisema hayo Jumanne ya jana tarehe Mosi Machi katika hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya kubathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw).

Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, adia na zawadi muhimu kabisa ya mab’ath na kubaathiwa Mtume (saw) kwa jamii ya mwanadamu ilikuwa ni kulingania “kutafakari na kutumia akili” na “kuitakasa nafsi na masuala ya kimaadili” kwa ajili ya kukabiliana na ujahilia. Ayatullah Khamenei ameashiria kuundika “Ujahilia wa Kisasa” katika ulimwengu wa Magharibi kwa sura pana na ya kuratibiwa na kusisitiza kwamba: Hii leo dhihirisho la wazi na kamili la Ujahilia wa Kisasa ni utawala wa kimafia wa Marekani ambao kimsingi ni utawala unaoibua na kupandikiza migogoro.

Kuachwa kutumiwa akili na hekima katika masuala ya jamii na nafasi yake kuchukuliwa na hisia na tajiriba katika maisha ya mwanadamu, ni miongoni mwa nembo za wazi za kurejea Ujahilia wa Kisasa katika jamii ya kimataifa. Ujahilia iwe ni katika kipindi cha kabla ya Uislamu katika ulimwengu wa Kiarabu au iwe ni katika zama hizi una utambulisho unaoshabihiana ambapo sifa kuu yenye ushirikiano ya ujahilia ni kuondolewa na kutotumiwa akili, mantiki na imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu.

 

Kwa maneno mengine ni kuwa, katika hali ambayo Waarabu katika zama za ujahilia walitumbukia na kunasa katika itikadi na vitendo vichafu na vya fedheha kutokana na kutokuwa na elimu na kutofungamana na sheria za Mwenyezi Mungu, hii leo jamii za Kimagharibi ikiwemo Marekani licha ya kujigamba na kutoa madai ya kuwa na elimu, teknolojia na maadili lakini kila lahdha zimekuwa zikizama zaidi na zaidi katika dhambi na ufisadi.

Nafasi ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ya madola ya Magharibi katika kuibuka na kujitokeza makundi ya kigaidi, mchango wa madola hayo katika kutokea akthari ya vita katika maeneo mbalimbali ya dunia, kukabiliana na mataifa yanayopigania uhuru na mamlaka ya kujitawala, ubaguzi wa rangi na mmomonyoko wa maadili ni sehemu moja tu ya Ujahilia wa Kisasa wa ustaarabu wa Magharibi ambao umekuwa ukienezwa na madola Magharibi ikiwemo Marekani kutokana na kuwa na nguvu ya kiuchumi na kihabari ulimwenguni.

 

Ni kwa msingi huo, ndio maana Ayatullah, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema kuwa, lengo kuu kabisa la Bwana Mtume (saw) la kubaathiwa kwake lilikuwa ni kukabiliana na ujahilia na akasisitiza kwamba, hii leo ule ule wigo wa ujahilia uliokuwako kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu unashuhudiwa kwa sura pana na iliyoratibiwa katika ulimwengu wa Magharibi unaojulikana kama uliostraabika ambao kimsingi umejengheka juu ya tamaa na uchu.

Ayatullah Khameneia amebainisha kwamba, tamaa, uchu, fedha, ubaguzi, kutumia teknolojia kwa ajili ya kuua wanadamu, kupora mali za mataifa dhaifu, utovu wa kimaadili, ufisadi, na mmomonyoko mkubwa wa kimaadili ni sifa na misingi mikuu ya ustaarabu wa Kimagharibi ambao kimsingi umechukua sura ya kisasa tu kwani ndiyo ule ule ujahilia ulikuweko kabla ya kuja na kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu.

Wakati huo huo, takwimu zinazotolewa na asasi na taasisi za kielimu zinaonyesha kuweko matatizo mengi ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kijamii na kimaadili na natija ya hayo, ni kuibuka wimbi la malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali na tawala zao barani Ulaya na hususan nchini Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali khamene, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Robert J. Ringer ni miongoni mwa wasomi ambao kwa kudiriki mmomonyoko wa kiutamaduni katika ulimwengu wa Magharibi anaamini kwamba, sababu ya hili ni kuweko mizizi ya ufisadi wa kimaadili. Anaandika kwamba, kusambaratika na kuporomoka Magharibi kunaweza kuainishwa katika jedwali la panda shuka. Athari ya kuporomoka Marekani katika miaka 50 ya hivi karibuni (baina ya mwaka 1912-1963) zilikuwa zikionekana miaka 137 iliyopita na athari za miaka 20 ya hivi karibuni zilikuwa zikionekana miaka 50 iliyopita.

Ni kwa muktadha huo, ndio maana Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema kuwa, kuna udharura wa kupata mafunzo na ibra za mab’athi kwa ajili ya kukabiliana na “Ujahilia wa Kisasa” na kusisitiza kuwa, “kuimarisha imani ya kidini”, “kupanua makundi ya waumini na yenye kusimama kidete katika maeneo mbalimbali ya dunia”, “umadhubuti na uimara wa mfumo wa Kiislamu”, “kuweko mipango ya hekima na busara” na “kutambua kwa mapana na marefu sifa za ujahilia wa kisasa” ni mambo ambayo hapana shaka kuwa, yataandaa uwanja na mazingira mwafaka ya kukabiliana vyema na ujahilia huu.